Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge mteule kuanza na hoja binafsi bungeni

388ca4c6bac4cca9149d2ea14104677f Mbunge mteule kuanza na hoja binafsi bungeni

Mon, 9 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MBUNGE Mteule wa Jimbo la Tarime Mjini, Michael Mwita amesema atapeleka hoja binafsi bungeni ili kuondoa sheria inayoruhusu mtaala wa elimu kubadilishwa muda wowote.

Mwita alisema hayo juzi wakati akizungumza katika mahafali ya saba ya kuhitimu darasa saba katika Shule ya Msingi Ghati Memorial yenye mchepuo wa kiingereza iliyopo kata ya Terat, jijini Arusha, ambapo wanafunzi 145 walitunukiwa vyeti.

Mwita ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shule za Ghati Memorial, Nyahiri na Mlimani nchini, alisema atawashawishi wabunge wenzake ili kupitisha hoja hiyo ambayo ana amini yakifanyika marekebisho itakuwa mkombozi katika sekta ya elimu.

Alisema hatua ya serikali kubadili mtaala wa elimu mara kwa mara inasababisha usumbufu kwa shule na wanafunzi na kushusha ufaulu.

"Mtaala wa elimu uliopo kwa sasa haukidhi mahitaji ya mhitimu, tunachotaka uboreshwe ili kumjengea mazingira bora mhitimu aweze kukabiliana na soko la ajira," alisema.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ndaro Nyahuga alisema jumla ya wanafunzi 145 walioanza darasa la kwanza wote wamehitimu elimu ya msingi shuleni hapo na ana imani wote watafaulu vizuri kutokana na historia ya shule hiyo kufaulisha wanafunzi wote kila mwaka.

Hata hivyo, alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara inayofanya wanafunzi kuchelewa kufika shuleni na kuiomba serikali kuzifanyia matengenezo barabara zote zilizopo jirani na shule hiyo ili ziweze kupitika nyakati zote ikiwamo msimu wa mvua.

Katika risala ya wahitimu iliyosomwa na mwenzao, Zara Suleiman waliishukuru shule hiyo kwa kuwapatia elimu bora.

Waliwataka wazazi kutokwepa jukumu la malezi ya watoto wao na kuwaachia walimu kwani baadhi ya wanafunzi wana tabia ya utoro inayosababishwa na ufuatiliaji hafifu wa wazazi.

Chanzo: habarileo.co.tz