Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge awapa wanafunzi mzuka kwa Samatta

14195 Pic+mbunge TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. KWA sasa shangwe imetawala kila kona nchini kutokana na straika wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji, kuongeza kasi ya kupasia nyavuni hivyo kuendelea kulitangaza soka la Bongo, ambapo mzuka huo ukamsukuma Mbunge Aysharose Mattembe kuwataka wazazi kuwaunga mkono watoto wao kushiriki michezo.

Aysharose, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, amesema michezo hasa soka ni ajira ya uhakika lakini, bado wazazi wamekuwa na msukumo hafifu kuhamasisha watoto wao hivyo kuwaacha wakipotea badala ya kuwaendeleza.

Akizungumza na wazazi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mlewa iliyopo wilayani Manyoni wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua Ilani ya CCM, alisema wazazi na walezi bado wana jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wanakuwa na nidhamu nzuri, lakini pia kuendeleza vipaji vya michezo.

Amesema mbali na kuwa michezo ni ajira ya uhakika kwa sasa duniani kote, pia imekuwa msaada mkubwa katika kudhibiti vitendo vya uhalifu ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya ambavyo vimekuwa vikiwaathiri vijana wengi wakiwemo wanafunzi.

Amewaasa wazazi waliofurika shuleni hapo, kutumia muda kufuatilia maendeleo ya shule na kugundua vipaji vya watoto na kuviendeleza, akitolea mfano wa Samatta na wachezaji wengine wanaoshiriki Ligi Kuu Bara na zile za Ulaya, ambao wamekuwa msaada kwa familia zao kupitia soka.

“Ndugu zangu michezo kwa sasa ndio inafuata baada ya elimu, ni muhimu sana kwa wazazi kufuatilia kwa karibu maendeleo ya elimu ya watoto wetu, tusiwaachie walimu peke yao hata sisi tuna jukumu hilo. Lakini, tusisahau michezo jamani, imekuwa kimbilio na ajira ya uhakika ya kuachana na umasikini. Wote tunamjua Samatta, Wayne Rooney na akina Neymar ambao kwa sasa ndio wameziinua familia zao kupitia mchezo wa soka. Tusiume vipaji ya watoto wetu, tuhakikishe tunaviendeleza lakini shule ni

muhimu sana,” alisema Mbunge Mattembe.

Katika ziara yake hiyo, Mattembe alikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali zikiwemo seti za jezi kwa mchezo wa soka na wanawake pamoja na michezo huku akiwataka wanafunzi kukomaa na masomo pamoja na michezo.

Pia, msaada kama hiyo ya jezi na mipira imekabidhiwa kwenye shule mbalimbali za sekondari na msingi zikiwemo za Miembeni, Kimadoi na Ilongero lengo likiwa ni kuendeleza michezo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz