Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge awaita wapinzani wadudu, apingwa

80116 Mbunge+pic

Tue, 15 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Masasi Mjini, Rashidi Chuachua (CCM) amewataka wananchi wa jimbo hilo kutowachagua viongozi wanaotokana na vyama vya upinzani kwa kuwa hawana tofauti na “wadudu”, lakini kauli hiyo imepingwa vikali.

“Sisi kama CCM hatupo tayari kufanya kazi na wadudu. Msituletee wadudu. Na hii wairekodi, nawaita wadudu. Tutafanya kazi na watu walio tayari kujenga nchi, si majungu na midomo,” alisema Chuachua, msomi wa lugha ya Kiswahili, wakati akihutubia wakazi wa Kata ya Mkuki.

Kauli hiyo imeibuka katika kipindi ambacho baadhi ya watu wanahusisha kauli za wanasiasa kuwa moja ya sababu za muitikio mdogo wa wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24.

Na baadhi ya watu waliojadili kauli hiyo wamefikia kuiita kuwa ya uchochezi, lakini mwanasiasa huyo aliiambia Mwananchi jana kuwa haoni tatizo.

“Hiyo itakuwa tafsiri zao tu. Mimi ni mwanasiasa nimetamka nikiwa kazini. Nimesema binadamu kamili ana utashi, issue (suala) yangu ni kwamba kila mtu anaona tunachofanya. Mwenye utashi anaweza kufafanua, akakosoa,” alisema Chuachua jana.

“Asiye na utashi hawezi kuona zuri wala baya. Hata mdudu hajui zuri wala baya. Kwa hiyo watu wanaweza kutumia tafsiri hii kwa namna wanavyotaka wao.

Pia Soma

Advertisement
Katika mitandao ya kijamii baadhi ya watu walishauri hatua zichukuliwe dhidi ya mbunge huyo.

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia alisema kitendo cha mbunge huyo ni ukosefu wa maadili na kutotambua athari zake katika kuchochea ubaguzi na machafuko baadaye.

“Muda wa kampeni haujaanza, pili kauli yake ndiyo sehemu ya chanzo cha watu kususia hata kujiandikisha,” alisema Mbatia ambaye ni mbunge wa Vunjo.

“Kwa hiyo, CCM itoe tamko la kukemea kauli hiyo. Haiwezekani tujiite Taifa la amani wakati wengine tunaitwa wadudu. Kama mimi ni mdudu ninaongoza wadudu.”

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo ole Ngurumwa alisema historia ya ubaguzi katika nchi zote zisizokuwa na utulivu, msingi wake ni maneno ya chuki na ubaguzi.

“Suala hili inabidi kukemewa kwa sababu wapinzani ni ndugu zetu, Watanzania wenzetu, wako kisheria, kikatiba na wako wengine wanahamia CCM. Kwa hiyo tukemee sote,” alisema.

Mbunge huyo akiongozana na madiwani wa jimbo hilo Oktoba 3, mwaka huu alianza ziara ya katika Kata 14 za jimbo hilo, akihamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kupiga kura ili kuwa na sifa ya kushiriki uchaguzi huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz