Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge atuma kilio cha korosho kwa Magufuli

34965 Mwambe+picMbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe ameainisha changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika suala la malipo ya korosho linaloendelea kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Ruvuma.

 

Mwambe amezitaja changamoto hizo jana Ijumaa Januari 6, 2019 katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari.

 

Kabla ya kuzitaja changamoto hizo, Mwambe amesema: “Nimeamua kutoa mrejesho wa yanayoendelea katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani kwa wakulima baada ya kufanya uchunguzi wangu binafsi kama mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Ndanda ambao na wao wako katika kilio cha kutolipwa.”

 

“Ifahamike kwamba, baadhi ya wakulima wanalipwa, wale wanaozalisha zaidi ya tani 1.5 wao hawalipwi wakiwemo makundi ya  wazee, wajane na warithi. Hatua hii ni  kuwaongezea uchungu wa maisha kwa kisingizio cha uhakiki,” amesema Mwambe.

 

Mbunge huyo amesema, “Wanahabari nawatuma taarifa hii ili kufikisha kilio cha wakulima wa korosho kwa Rais John Magufuli.”

 

Baada ya maelezo hayo, Mwambe alizitaja changamoto hizo ni kuwa utaratibu wa malipo umekuwa wa kusuasua tofauti na taarifa alizopewa Rais Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

 

Amesema kuwa kuna viashiria vya rushwa wakati wa mchakato wa kazi ya uhakiki kutoka kwa wahakiki na wakulima wamegawanywa kwenye makundi jambo linalowafanya kuwa wanyonge.

 

Mbali na hilo, amedai kumekuwapo na matumizi makubwa ya nguvu kutoka vyombo vya ulinzi na usalama na suala hilo lipo katika maeneo mengi, kubwa zaidi ni tukio lililotokea Nachingwea ambapo viongozi wa vyama vya msingi wamepigwa.

 

Kwa mujibu wa Mwambe, changamoto hizo zinaweza kuleta athari kwa halmashauri kushindwa kujiendesha kwa sababu zinategemea kwa kiasi kikubwa mapato yatokanayo na mazao ikiwemo korosho.

 

Mbali na hilo, kuharibika kwa korosho zilizopo maghalani kwa kunyeshewa na mvua, hasa zile zilizopo mikononi mwa wakulima na hivyo kupoteza ubora wake ambao ndio sifa kuu ya zao hilo.

 

“Wakulima kudhalilishwa kwa kushindwa kujimudu maisha yao ya kawaida, mfano kulipia ada za watoto na michango mbalimbali. Hii pia itasababisha kushuka kwa elimu,  lakini pia wakulima hawahawa watashindwa kuandaa mashamba yao kwa ajili ya msimu ujao.”

 

Katika taarifa hiyo, Mwambe amemaliza kwa kumuomba Rais Magufuli kutembelea mikoa ya Kusini na kuwapa wananchi nafasi ya kuzungumza ili ajionee na kusikia  mwenyewe  kinachoendelea kwa lengo la kumsaidia mkulima na si vinginevyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz