Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge ataka wananchi wapewe elimu ya mikopo

Db1f81a95213d5cc20f37461dad1793f.jpeg Mbunge ataka wananchi wapewe elimu ya mikopo

Tue, 12 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MBUNGE Viti Maalum mkoa wa Dodoma, Fatma Tawfique ameiomba serikali

kutoa elimu ya usimamizi wa fedha za mikopo ya vikundi

inayotolewa na halmashauri nchini ili kuepusha kuitumia kinyume malengo yaliyokusudiwa.

Pia ameomba watunga sera kuongeza mtaala wa elimu ya namna ya matumizi ya fedha kuanzia shule za awali ili kuwajengea wanafunzi fikra za kujiajiri wenyewe wanapohitimu masomo yao.

Alitoa wito huo juzi wakati akifungua warsha ya vijana ilioandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Endless Succes Foundation kwa lengo la kuwainua kiuchumi na kuacha dhana potofu ya kusubiri kuajiriwa.

Toufiq alisema serikali imeweka utaratibu mzuri wa kutoa mikopo kwa

vijana, watu wenye ulemavu na wanawake, lakini wengi hasa vijana wanashindwa kuitumia vizuri kwa sababu hawana

elimu ya biashara na matumizi sahihi ya fedha hizo.

"Ifike wakati vijana wapatiwe elimu ili kujiinua kibiashara hasa ikizingatiwa taifa lipo kwenye uchumi wa kati, vijana wanapaswa kuelimika kibiashara ili wasonge mbele katika biashara wanazokusudia kufanya." alisema.

“Ikifanyika hivyo vikundi vingi vya vijana vitanufaika na mikopo inayotolewa na serikali kwa ajili ya kuendesha biashara zao ambazo wamekusudia kufanya katika maeneo mbalimbali, alisema.

Mbunge huyo alisema lengo la serikali ni kuona makundi ambayo imelenga kuyasaidia kupitia mikopo yanapiga hatua za maendeleo na si kurudi nyuma.

Kuhusu kuongezwa mtaala wa elimu ya biashara kuanzia shule

za msingi, alisema itasaidia

kwa kiasi kikubwa wahitimu nini wanatakiwa kufanya pale

wanapohitimu masomo yao.

"Elimu ya biashara ikianzia shule ya msingi itawajengea wanafunzi uwezo wa kuchagua nini afanye pale atakapohitimu masomo yake," alisema Toufique.

Mkurugenzi wa Endless Succes Foundation, Amina Feruz alisema lengo la warsha hiyo ni kutoa elimu kwa vijana juu ya namna wanavyoweza kujiajiri wenyewe ikiwamo kusimamia fedha wanazokopeshwa katika vikundi vyao.

Alisema taasisi hiyo inalenga kuona vijana wanaachana

na fikra potofu ya kusubiri kuajiriwa wanapohitimu masomo na badala yake wafikirie kujiajiri kwa sababu fursa zipo.

“Hivi sasa taifa liko katika uchumi wa kati na vijana ndio taifa la kesho hivyo hakuna sababu ya kukaaa kusubiri ajira peke yake badala yake wanapaswa kujishughulisha na ujasiriamali wa vitu mbalimbali,” alisema.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St John, Janet Madege alisema

elimu waliyowapa itawasaidia kufanya biashara mbalimbali badala ya kusubiri ajira.

Chanzo: habarileo.co.tz