Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge amkingia kifua Rais Samia, asema…

Mbunge Ditopile Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mariam Ditopile.

Fri, 30 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mariam Ditopile amewataka wanasiasa nchini kuacha kubeza na kupotosha jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kukopa nchi kwa kugharamia miradi ya maendeleo.

Mbunge huyo anayewakilisha Mkoa wa Dodoma amesema hayo leo Ijumaa, Desemba 30, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Amesema kitendo cha Tanzania kukopesheka kimeonesha jinsi gani nchi inayoongozwa na Rais Samia inaaminiwa.

Ditopile ametoa kauli hiyo kipindi ambacho deni la Taifa limefikia Sh 91 trilioni huku Rais Samia hivi karibuni alieleza Serikali yake itaendelea kukopa kwa ajili ya kugharamikia miradi mbalimbali ya wananchi.

Katika mkutano wake na wanahabari, Ditopile amesema, nchi haikopesheki tu hovyo kuna mambo ya kiuchumi lazima yazingatiwe.

Amesema jambo la kwanza inaangaliwa na kupitiwa taarifa ya ustahimilivu wa deni kwa miaka 10 iliyopita na baada ya kuridhika na ustahimilivu huo pili inaangaliwa matarajio ya miaka 20 ijayo.

“Mchakato huo unaangaza uwiano wa pato la mwaka na uuzaji wa bidhaa zetu nje pamoja na pato la mwaka na deni la Taifa ambapo ili ufuzu viwango vya kukopesheka Tanzania inapaswa uwiano huo usizidi asilimia 55,” amesema

Kwa takwimu za Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) zinaonesha uwiano wetu Tanzania upo chini ya asilimia 30 ambayo ni hali nzuri na itachukua zaidi ya vizazi viwili kufikia hiyo asilimia 55 na zaidi ya vizazi vinne kufikia asilimia 75 ambacho ndio kiwango hatari cha ukopeshaji.

“IMF na Benki ya Dunia zimeipongeza nchi yetu kwamba pamoja na mlipuko wa Uviko-19 na vita ya Urusi na Ukraine uchumi wetu umekua mstahimilivu na haujatetereka hata kidogo,” amesema

“Niwasihi Watanzania wenzangu tuendelee kumuombea na kumuunga mkono Rais wetu. Niwaombe Watanzania kuwapuuza wanasiasa ambao wanafanya upotoshaji kuhusu mikopo ambayo Serikali inakopa na kwamba mikopo hiyo inakopwa kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa Watanzania,” amesema

Ingawa Ditopile hajamtaka mtu anayekosoa mikopo hiyo, lakini mapema mwaka huu, aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai alitahadharisha mikopo ya Serikali kwamba inaweza kusababisha nchi ikapigwa mnada.

Kauli hiyo ilimwingiza matatizoni kwa wanachama wa CCM wakiwemo wabunge kumkosoa vikali na kumtaka kujitathimini ikiwa anastahili kuendelea kuongoza Bunge.

Januari 6 mwaka huu, Ndugai alitangaza kujiuzulu uspika na nafasi yake kwa sasa inaongozwa na Dk Tulia Ackson aliyekuwa naibu wake.

Aidha, Ditopile amesema, safari za Rais Samia nje ya nchi zimesaidia kuifungua nchi na kuvutia wawekezaji wengi kumiminika kuwekeza Tanzania.

Amewataka Watanzania kuendelea kufanya kazi na kumuunga mkono Rais Samia kwani ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake ametekeleza mambo makubwa katika kila sekta ikiwemo elimu, afya na maji.

Chanzo: Mwananchi