Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge akabidhi mifuko 430 ya saruji ujenzi wa madarasa

64d47fa5e35f5ab800bf2c923846591d Mbunge akabidhi mifuko 430 ya saruji ujenzi wa madarasa

Wed, 20 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MBUNGE wa Jimbo la Chamwino wilayani Chamwino mkoani Dodoma, Deogratius Ndejembi ametoa msaada wa mifuko zaidi ya 430 ya saruji kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika jimbo hilo.

Ndejembi ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora, alitoa msaada huo hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kutembelea jimbo hilo katika kata za Haneti, Zajilwa na Itiso.

Aidha Ndejembi pia alichangia zaidi ya milioni 15 kwa jili ya ujenzi na ukarabati wa baadhi ya vyumba vya madarasa katika baadhi ya miradi ya elimu kwenye kata hizo tatu za jimbo lake.

Ndejembi alichangia saruji hiyo ili kuunga mkono juhudi za wananchi wa kata hizo tatu kwenye jimbo lake katika kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa na wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaanza masomo.

“Wananchi, ubunge huu nilionao ni mali yenu hata mshahara ninaopata ni wenu, hivyo siwezi kuona watoto wetu wanakosa masomo na mimi nikanyamaza, nimeona nifike ili tushirikiane kukamilisha vyumba hivi vya madarasa ili watoto wetu wote waanze masomo,”alisema.

Kati ya mifuko hiyo, Ndejembi akiwa katika kata ya Haneti alichangia mifuko 100 ya saruji ili kukamilisha ujenzi wa vyumba madarasa ya sekondari ya Haneti.

Akiwa katika Kijiji cha Gwandi pia alichangia mifuko 100 ya saruji na fedha taslimu Sh milioni mbili kwa ajili ya kukarabati vyumba viwili vya madarasa ya shule mpya ya msingi inayotarajiwa kuanzishwa hapo.

Ndejembi pia alitoa Sh milioni 10 kwa lengo la kuchangia juhudi za wananchi wanaojenga shule mpya ya sekondari ya kata ya Zajilwa. Pia Mbunge huyo alichangia mifuko 100 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya shule ya sekondari Itiso.

Ndejembi akiwa katika kitongoji cha Mditi pia alichangia fedha taslimu Sh milioni moja na mifuko 30 ya saruji kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa ya Shule ya Msingi Ndejembi.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Zajilwa, Gefile Tamba alisema kata hiyo haina shule ya sekondari ambapo watoto hulazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 16 kwenda Shule ya Sekondari ya Kata ya Segala kupata elimu.

Tamba alisema kutokana na tatizo hilo wameanzisha michango kwa ajili ya ujenzi wa shule ya kata yao ya Zajilwa ili kuhakikisha inaanza kutoa huduma ya masomo katika mwaka wa masomo 2021/2022 shule ambayo itayaosaidia watoto wa vijiji vya Magungu, Zajilwa na Gwandi.

Chanzo: habarileo.co.tz