Dodoma. Mbunge wa Tanga Mjini (CUF), Mussa Mbarouk amehoji sababu za madiwani wa chama hicho mjini Tanga waliohamia CCM kuendelea na nafasi zao akitumia neno, “wamehama na nafasi zao kwenda CCM.”
Mbarouk ameeleza hayo leo Jumanne Februari 4, 2020 bungeni mjini Dodoma katika mjadala wa taarifa za utekelezaji wa shughuli za Kamati za Bunge za Utawala na Serikali za Mitaa, Katiba na Sheria pamoja na Sheria Ndogo.
Amesema kwa ufahamu wake moja ya sifa ya kupoteza udiwani ni iwapo mhusika atahama chama kimoja kwenda kingine, kufungwa zaidi ya miezi sita na kufanya biashara na halmashauri bila kutangaza.
Januari 26, 2020, siku 11 baada ya madiwani wanne wa CUF kutangaza kujiuzulu nyadhifa zao na kujiunga na CCM, waliibuka na kushiriki kama wajumbe halali wa baraza la madiwani wa halmashauri ya jiji hilo na kupitisha bajeti ya Sh66.1 bilioni kwa ajili ya mwaka wa fedha 2020/21.
Uongozi wa jiji la Tanga ulidai kuwatambua madiwani hao wakati chama chao (CUF) kikiwakana.
Madiwani hao walijiuzulu na kupokelewa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally Januari 15, 2020 akiwa ziarani mkoani Tanga.
Habari zinazohusiana na hii
- Madiwani waliojiuzulu CUF, washiriki mkutano baraza la jiji Tanga, wapitisha bajeti
- Madiwani wanane CUF wahamia CCM, wamtaja Magufuli
Katika maelezo yake bungeni, mbunge huyo amesema cha kushangaza ni kutofuatwa kwa sheria kwakuwa madiwani hao bado wanaingia katika vikao vya madiwani, wanalipwa posho na pesa nyingine mwisho wa mwezi.
“Na hili jambo linapitishiwa sasa wakitokea wasamaria wema wakifungua kesi kwamba bajeti hiyo iliyopitishwa si halali si ina maana tutaathiri wananchi wa Tanga sababu itabidi halmashauri isimame,” amesema Mbarouk.
Amesema si mara ya kwanza suala hilo kutokea, akibainisha kuwa mwaka 2014/15 diwani mmoja alifanya kitendo kama hicho na kutangazwa na mkurugenzi kuwa ataendelea kuwa diwani na atapewa kiinua mgongo.
Akitoa taarifa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo amesema tatizo hilo lilijitokeza Kinondoni mwaka 2019 ambapo diwani wa viti maalum kupitia Chadema alihamia CCM lakini kikao kilichofuata akawa CCM licha ya kuwa wanajua kuwa majina yanaenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).