Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge afananisha kuwekeza kwenye elimu na upatu

Tue, 30 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Kahama Mjini (CCM),  Jumanne Kishimba amesema changamoto ya ukosefu wa ajira nchini inafanya fedha wanazowekeza wazazi katika elimu ya juu kufanana na mchezo wa upatu.

Mbunge huyo alitolea mfano kuwekeza fedha hizo kuwa ni sawa na wale waliowekeza  katika kampuni ya kusimamia shughuli za upatu kwa mtindo wa kupanda na kuvuna fedha (Deci).

Ametoa kauli hiyo  bungeni jijini Dodoma leo Jumanne Aprili 30  wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Kishimba amesema tatizo la ajira nchini ni kubwa kuliko hata la Katiba mpya na kutaka iundwe tume kuchunguza mfumo wa elimu nchini kama alivyoshauri Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Amesema hivi karibuni zilitangazwa ajira katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  wakaenda watu 40, 000 kwenye usaili  wakati waliohitajika ni 70 tu nakueleza  kwamba suala ni la kukatisha vyuo vinavyozalisha wanafunzi hao.

Amesema mtu anauza mifugo yake na kwenda kusomesha wanafunzi lakini wanawaacha wakazunguke mtaani na shahada waliyoipata.

Related Content

‘Mimi mwenyewe ni muathirika wa shahada, ninao watoto sita wana shahada.  Watunga sera tukubaliane kuwa vyuo vikatafute ajira waseme NSSF tumepata ajira mshahara ni 500,000. Sasa tunaanza kusajili nipe Sh 5milioni ajira hii hapa.”

“Linaweza kuwa suala la kuchekesha lakini hali ni mbaya sana mitaani watu wana shahada kila kona.”

“Ni muda wa watunga sera kuangalie upya mfumo wetu wa elimu. Ni kweli nani alifanya utafiti  wa binadamu unahitaji kila mwaka darasa moja? Kama yupo atuambie. Nafasi za ajira wakati huu hakuna unachukuliwa mtoto wako ana miaka 17 unarudishiwa ana miaka 25  akisharudishwa unaambiwa akajitegemee,” amesema.

Amesema ni vyema watunga sera wakaruhusu mtu kusoma  madarasa kati ya mawili hadi matatu kwa mwaka mmoja ili wanafunzi waweze kumaliza mapema shule.

Amesema ni muhimu kuundwa tume itakayoangalia mfumo wa elimu nchini ambayo itashirikisha watu wa kada mbalimbali.

“Ukienda kijijini na kuuliza mtoto yupi ana faida wanakwambia mtoto ambaye hajasoma, anafuata wa darasa la saba, wa kidato cha nne na sita na wa shahada hana faida ni kama viazi vilivyoshindwa kuiva hawezi kufanya kazi yoyote na hawezi kulima,” amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz