Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge adai wapinzani wanakataa maendeleo

10751 Pic+mbunge TanzaniaWeb

Wed, 8 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hanang. Mbunge wa viti maalumu wa Mkoa wa Manyara, Martha Umbullah (CCM) amewataka wananchi wa Kata ya Masakta wilayani Hanang’ kutowachagua wapinzani kwani wamekuwa wakipinga maendeleo, hivyo kuwarudisha nyuma wananchi.

Umbullah aliyasema hayo jana wakati akimnadi mgombea udiwani wa Kata ya Masakta, Marco Kia (CCM) katika mkutano uliofanyika Kijiji cha Masakta.

Alisema mara nyingi viongozi wa upinzani wakiwemo wabunge na madiwani wamekuwa wanapinga bajeti ya maendeleo bungeni na halmashauri wakati wa kupitisha bajeti, hivyo hawapaswi kuchaguliwa ila kunyimwa kura.

Alisema wakazi wa Kata ya Masakta wanapaswa kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa kumchagua diwani kupitia CCM, kuliko kufanya makosa kwa kumchagua mgombea wa Chadema ambaye alisema atakuwa anapinga maendeleo.

“Kia ni kijana mdogo mwenye kupenda maendeleo, hivyo tutumie fursa hii kwa kumpa kura zote za ndiyo ili aweze kuwatumikia tena wananchi wa kata ya Masakta ambao ni wapenda maendeleo,” alisema Umbullah.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hanang’, Mathew Darema aliwaomba wananchi wa kata hiyo kumchagua mgombea wa CCM kwa kuwa ile kero yao ya muda mrefu ya kupatiwa soko na mnada imeshapatiwa ufumbuzi.

“Juzi tu hapa Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Hanang’ kwa kauli moja wamepitisha uanzishaji wa soko na mnada wa Masakta tuliahidi na tukatekeleza CCM,” alisema Darema.

Mgombea Kia alitoa ahadi ya kuendelea kuwatumikia wananchi wa eneo hilo kwa kuendeleza pale alipoishia, kwani CCM atakuwa na nafasi nzuri zaidi tofauti na Chadema alikohama.

“Huku CCM ndiyo kwenye mambo yote jamani, kule Chadema nilipitiwa tu ndugu zangu, naombeni kura zote za ndiyo tusaidiane kufanikisha maendeleo kwa faida ya kata ya Masakta,” alisema Kia aliyejiuzulu udiwani na kuhama Chadema.

Chanzo: mwananchi.co.tz