Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge Sugu aimba 'Mbeya Ndiyo Inanitesa'

9347 Sugu+pic TZW

Sat, 16 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ameamua kutumia kipaji chake cha muziki  kueleza matatizo anayopitia kwa sasa katika siasa.

Mbilinyi, ambaye kisanii anajulikana kama Sugu, ametoa kibao kipya kinachoitwa "#219, Juni 15, 2018", akirejea namba aliyokuwa akitumia jela baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano kwa kosa la kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Katika wimbo huo wenye beti tatu, Sugu anazungumzia harakati zake za kisiasa zilizosababisha afungwe gerezani akiwa mfungwa namba 219.

“Muziki sikuuchagua, bali ulinichagua, nikafanya kweli na dunia ikanijua, nilichofanya kwa hili gemu mnakijua," anasema katika moja ya mashairi.

"Mbeya ndiyo inanitesa (wanaitaka Mbeya), najua Mbeya ndiyo inanitesa. Lakini bado napenda Mbeya inavyonitesa.

“Siasa sikuichagua, amini usiamini siasa ndiyo ilinichagua na iliponichagua Mbeya wakanichagua, kwa mara nyingine tena dunia ikanitambua na wale wasioamini wakaamini imeshakuwa.”

Sugu alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano Februari 26, 2018 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Desemba 30, 2017 eneo la Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Mei 10, 2018 Sugu aliachiwa kwa msamaha wa Rais na kutoka katika Gereza Kuu la Ruanda mkoani Mbeya alikokuwa akishikiliwa.

Sugu, ambaye aliingia kwenye muziki kwa jina la ll Proud katikati ya miaka ya tisini, alijipatia umaarufu kutokana na kuimba muziki wa rap kwa kutumia lugha ya Kiswahili, tofauti na wasanii wengine waliokuwa wakirap kwa Kiingereza.

Sehemu kubwa ya mashairi yake ilikuwa ni ujumbe wa kisiasa.

Baadhi ya nyimbo hizo ni pamoja na "Ni Mimi", "Itikadi", "Ndani ya Bongo", "Nje ya Bongo" na wimbo wa hivi karibuni wa "Freedom".

Alipambana na baadhi ya wanasiasa wakati alipojaribu kuingia kwenye kampeni ya kupambana na ugonjwa wa Malaria na baadaye kuamua kuingia kwenye siasa.

Alijiunga na Chadema na baadaye kupewa nafasi ya kugombea ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini mwaka 2010 na kushinda na katika uchaguzi uliopita, Sugu aliweka rekodi ya kuwa mbunge aliyechaguliwa kwa kura nyingi kuliko wabunge wote nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz