Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge Nusrat amtupia zigo lote Mnyika

Nustart Chadema.jpeg Mbunge Nusrat amtupia zigo lote Mnyika

Sun, 6 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbunge wa viti maalumu aliyevuliwa uanachama wa Chadema, Nusrat Hanje amedai fomu ya kugombea ubunge huo alipelekewa mahabusu na katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Hanje alitoa kauli hiyo juzi wakati akihojiwa na wakili wa Chadema, Hekima Mwasipu iwapo anaitambua fomu namba 8 (a) inayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Aliendelea kueleza kuwa alisaini fomu hiyo kisha Mnyika akaondoka nayo na kwamba ndiye anayejua taratibu nyingine zilizofuata.

Alidai wakati huo alikuwa Katibu Mkuu wa Vijana (Bavicha), hivyo alikuwa akisaini nyaraka mbalimbali na kwamba hata alipokuwa mahabusu alikuwa akipelekewa kuzisaini.

“Hivyo hata nilipoletewa fomu hiyo sikushangaa,” alidai Hanje wakati akihojiwa na wakili Mwasipu. Pia Wakili Mwasipu alimuhoji kama anafahamu fomu hiyo ipo ofisi ya katibu mkuu wa Chadema, naye akajibu fomu anaifahamu, lakini hakumbuki ni fomu namba ngapi.

“Ni sahihi hiyo fomu lazima ukaapishwe na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo?” alihoji wakili huyo na Hanje kujibu kuwa anafahamu.

Akiendelea kujibu maswali ya wakili huyo, Hanje alikiri kuwa Novemba 23, 2020 usiku alitolewa gerezani baada ya DPP kuiondoka kesi yake.

“Muda mfupi baada ya kutolewa gerezani, nilipigiwa simu na Mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe na katibu mkuu, John Mnyika na wakaniuliza kamanda upo fiti? nikawajibu niko fiti, wakaniambia tarehe 24 Novemba 2020 (yàani kesho yake) natakiwa kwenda kuapishwa bungeni kama mbunge wa viti maalumu,” alidai.

Alidai mchakato wa uteuzi na kuapishwa kwake ulifanikishwa na Mbowe na Mnyika, lakini akaeleza kushangaa sasa wanavyomgeuka na kumkana.

Hanje alidai akiwa mahabusu katika gereza la Isanga Dodoma, alikokuwa akishikiliwa kutokana kesi ya jinai ya kufanya mikusanyiko isiyo halali, alikuwa akitembelewa na viongozi mbalimbali wa Chadema akiwemo Mbowe na Mnyika.

Madai hayo ya Hanje yanaonekana kujibu madai yaliyotolewa na viongozi wa Chadema hususan Mbowe na Mnyika ambao wamekana kuhusika wala kutambua uteuzi wao.

Novemba 25, 2020, siku moja baada ya wabunge hao kuapishwa, Mnyika aliitisha mkutano na waandishi wa habari kuelezea hatua za kinidhamu dhidi yao na kutoa taarifa ya kuwaita kuhojiwa na Kamati Kuu ya chama hicho.

Mnyika alieleza chama hicho kupitia vikao vyake hakijawahi kupeleka orodha ya majina yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiwa imesainiwa na Katibu Mkuu kama sheria inavyoelekeza, wala kuwapendekeza kupitia vikao vya chama.

Alidai mchakato wa uteuzi wao umefanikishwa na mfumo (Serikali na vyombo vyake kwa kushirikiana na Bunge), huku akitoa mfano wa Hanje kuwa alitolewa na mfumo mahabusu Novemba 23, 2020 usiku ili kesho yake aende kuapishwa.

Alihoji kuwa fomu yake aliijaza lini na hakimu aliyemuapisha kama sheria inavyoelekeza alikuwa wapi, na kwamba inadhihirisha ni kazi ya mfumo.

Hanje ni mmoja wa wabunge 19 waliofungua kesi kupinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022, kutupilia mbali rufaa kupinga uamuzi wa Kamati Kuu wa Novemba 27, 2020 kuwafukuza uanachama kwa tuhuma za kuapishwa kuwa wabunge bila ridhaa ya chama.

Katika shauri hilo la mapitio ya mahakama (Judicial Review), namba 36 la mwaka 2022 wabunge hao wanadai walifukuzwa isivyo halali kwa kuwa hawakupewa haki ya kusikilizwa, hivyo wanaiomba mahakama itengue uamuzi huo.

Wakati akihojiwa na wakili Kibatala kuhusu madai yake yaliyomsukuma kufungua kesi hiyo na wenzake, Hanje alidai hawakupewa fursa ya kusikilizwa Baraza Kuu na kwamba walipewa nafasi ya kuomba radhi pekee.

Hata hivyo, alikiri aliwasilisha sababu zake na kuzitolea ufafanuzi na anatambua kuna namna mbili za kusikilizwa, kwa mdomo na kwa maandishi.

Alidai kwa kuwa waliitwa, walipaswa kupewa nafasi ya kusikilizwa kwani isingewezekana kufafanua malalamiko yake kwenye kurasa tano.

Pia alikana baadhi ya maelezo kwenye muhtasari wa kikao cha Baraza Kuu wa Mei 11, 2022 akidai kuna maelezo mengine ambayo hayatambui na kwamba amekuwa katika sekretarieti wakiongozwa na Mnyika na kuna mambo mengine wamekuwa wakitengeneza.

Shauri hilo litaendelea Novemba 8, ambako itakuwa zamu ya Cecilia Pareso kuhojiwa na Novemba 9 atahojiwa Jesca Kishoa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live