Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge Mattembe awasaidia wanafunzi wasilale kwenye mikeka

Mon, 22 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe amepewa tuzo na cheti cha utendaji kazi bora katika jamii ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuboresha miundombinu ya Shule ya Sekondari ya  Mwanamwema Shein.

Mbunge huyo amekabidhiwa tuzo hiyo na uongozi wa  shule hiyo mbele ya wanafunzi na wazazi, akiwa kwenye ziara shuleni hapo kujionea mazingira, huku akikabidhi vitanda vyenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 40  kwa uongozi wa shule hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo na cheti maalumu cha shukrani, Mkuu wa shule hiyo, Zainabu Mtinda alisema Mattembe amekuwa akifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wanafunzi wa shule hiyo  wanasoma katika mazingira salama na tulivu.

"Amekuja hapa mara kadhaa na kila anapokuta mambo tofauti anarudi na ufumbuzi wake, ameshatuletea vitu mbalimbali na leo ametuletea vitanda 20, huu ni msaada mkubwa sana na wanafunzi wetu wataondokana na changamoto ya kulala kwenye mikeka.”

"Tumewaza sana ni kitu gani tutakupa ili kukutia moyo, wazazi na wanafunzi wakasema hii tuzo na cheti kitakuwa ukumbusho wa miaka mingi kwani kila ukikitazama utakumbuka hiki kikubwa ulichotupatia. Tunakushukuru sana na tutakuombea kwa Mungu azidi kukubariki," alisema mwalimu huyo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Singida, Eliah Digha alimpongeza Mattembe kwa kujitoa kwa ajili ya wananchi wa Singida na kwamba moyo huo unapaswa kuigwa na wabunge wengine.

Amewataka wanawake na vijana kuendelea kumtumia Mbunge huyo na kumpa ushirikiano wa hali na mali kwa kuwa ana dhamira njema na wananchi na sio mtu wa kujali maslahi BINAFSI kama wengine.

"Huyu Mattembe ndio mtu wa kumshika mkono. Anahudumia mkoa mzima bila upendeleo. Leo utasikia ametoa msaada na kufanya ziara Ikungi, kesho Mkalama mara yuko Iramba na hawa ndio watu tuliokuwa tunawataka. Hana makundi wala husikii fitna kwa huyu ni kazi kazi tu," alisema Digha.

Chanzo: mwananchi.co.tz