Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge Malinyi aeleza adha ya wananchi wake

62e829af6cacd07c6ff1172f719c6700 Mbunge Malinyi aeleza adha ya wananchi wake

Tue, 9 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MBUNGE wa Malinyi (CCM), Antipas Mgungusi ameelezea namna Wananchi wake wanavyotaabika kwa kutumia mitumbwi kufika Malinyi mjini baada ya barabara kutopitika wakati wote hasa msimu huu wa mvua.

Mbunge huyo, aliiomba serikali kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo, ikiwemo kuongeza idadi ya makalavati yatakayochepusha maji.

Katika swali lake la nyongeza, alisema sehemu ya barabara ya Lupiro, Malinyi ,Londo hadi Namtumbo, yenye urefu wa kilometa 296, katika Kijiji cha Misegese kufika Malinyi mjini haifikiki wala kupitika kipindi chote.

Alisema mvua inaponyesha kwa siku moja, wakazi wa maeneo hayo hulazimika kutumia mitumbwi kufika Malinyi Mjini huku magari yakiwa hayafiki kabisa.

"Sasa mkandarasi aliyepo anaweka kalavati moja badala sita au saba yanayotakiwa amepewa kazi ya kuinua tuta kwa mita 200 badala ya kilometa moja,"alisema.

Katika swali lake hilo, alihoji kuwa serikali haoni ya haja ya kumuongezea uwezo kulingana na uhitaji mkandarasi, pia alihoji kama Waziri yupo tayari kuongozana naye kwenda Malinyi kujionea hali halisi ya miundombinu na kutafuta suluhisho la pamoja.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alihoji ni serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hiyo ambayo ipo katika Ilani ya CCM 2020.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya, alisema barabara hiyo imekuwa ikiuliziwa na wabunge wanufaika wa barabara hiyo na atafanya ziara ili kufanya utatuzi.

Alisema atazungumza na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ili kuangalia tatizo lililopo na afanye kulingana na matakwa yaliyopangwa.

Naibu Waziri huyo alisema barabara hiyo ni sehemu ya barabara kuu ya Mikumi – Kidatu – Ifakara – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha yenye jumla ya kilometa 547 ambayo inaunganisha mikoa ya Morogoro na Ruvuma.

Alisema serikali kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hiyo Tanroads imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2018.

Alisema ujenzi wa sehemu ya Kidatu – Ifakara kilometa 66.9 kwa kiwango cha lami pamoja na daraja la Ruaha Mkuu bado unaendelea.

Alieleza kuwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa sehemu iliyobaki ikiwemo ya Lupiro – Malinyi – Londo – Namtumbo zinaendelea kutafutwa na serikali.

Alisema katika mwaka wa fedha 2020/21 jumla ya Sh milioni 720 na Sh. milioni 377.2 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo katika mikoa ya Morogoro na Ruvuma mtawalia ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.

Chanzo: habarileo.co.tz