Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge Kishimba aibuka na kituko kingine bungeni

83593 Pic+kituko Mbunge Kishimba aibuka na kituko kingine bungeni

Thu, 14 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Kahama Mjini (CCM), Jumanne Kishimba amewahi kusema bungeni kuwa Serikali ihalalishe matumizi ya bangi kwa madai kuwa ni malighafi ya kutengeneza dawa za binadamu.

Kishimba alitoa ushauri huo Mei 20 alipokuwa akichangia mjadala wa Bajeti ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.

Jana hakuwa tofauti sana alipokuwa akichangia katika Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2019/2020.

Alisema elimu ya Tanzania ni sawa na kifungo kwa sababu wahitimu wakihitimu wanakosa kazi za kufanya.

“Ukienda kwenye familia zilizoathirika kwenye suala hili la elimu ukasema elimu ni ufunguo wa maisha, watasema hapana elimu ya Tanzania ni kifungo kigumu cha maisha, unafungwa wewe, anafungwa mtoto, anafungwa mama na fedha zako ulizomgharamia zinakuwa zimeenda bure,” alisema.

Kishimba akichangia hoja hiyo ya elimu katika mjadala wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021.

Ilipofika zamu yake ya kuchangia hoja, akisema anatoa ushauri kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ianzishe mtalaa kwa wanafunzi wanaotoroka shuleni, wafundishwe na walimu waliotoroka enzi wanasoma, lakini wakafanikiwa.

Kishimba alianza kwa kuiomba wizara hiyo kufikiria upya utaratibu wa wanafunzi wanaotokana na familia za wafugaji, wakulima na wafanyabiashara ndogo.

Alisema kwa kawaida wanafunzi wakienda shuleni asubuhi, huanza na kukimbia mchakamchaka hadi saa 4:00 asubuhi ndipo wanaingia darasani kusoma.

“Kwanini watoto wasiende shuleni saa 5:00 asubuhi wakiwa wameshafanya kazi za nyumbani tayari.

“Wakifanya hivyo watarudi saa 10:00 jioni baada ya kusoma.

“Wanadamu wote sawa, lakini si Watanzania wote ni sawa. Utaratibu huu wa kwenda shuleni asubuhi ni wa Ulaya, wakati mwingine kukiwa na baridi kali wanaweza kulala hukohuko hata siku tatu,” alisema.

Alidai Ulaya wanafanya hivyo kwa sababu hawana kazi za kufanya, lakini Tanzania kuna kazi za kufanya nyumbani na kwamba kama wakiamua wanafunzi waanze kwenda shuleni saa 5:00 baada ya kazi za nyumbani, wataweza kuzalisha.

“Tanzania tuna wanafunzi karibu milioni nne, wakizalisha kilo moja ya mahindi kila mmoja watainua uchumi na watapata elimu ya kutosha ili wanapomaliza elimu ya chuo kikuu hawatakuwa na tatizo lolote la kurejea kijijini,” alisema mbunge huyo.

Alisema wizara inapambana na watoto watoro shuleni, lakini hao watoro wapo wengi waliofanikiwa baada ya kujitambua.

“Mheshimiwa mwenyekiti tuwe na mtaala wa watoro na watu wazuri. Leo tunashuhudia watu watoro wakifanya mambo makubwa. Leo tuna wanamichezo, wanamuziki na bahati, huku bungeni mheshimiwa mwenyekiti tuna wabunge zaidi ya 50 ni watoro, lakini wana mafanikio mazuri sana kwenye majimbo yao. Kwa ridhaa yako kama utakubali, nitaje hata 10 (wabunge),” alisema Kishimba.

Hata hivyo, alikatishwa na taarifa iliyotoka kwa mbunge wa Itilima (CCM), Njalu Siyanga aliyesema Kishimba naye hakumaliza shule ya msingi, lakini alifanikiwa sana kuchenjua dhahabu na mwaka 1992, alianzisha ununuzi wa pamba hapa nchini

Akijibu taarifa hiyo, Kishimba alikiri kuwa hakumaliza shule ya msingi na kwamba aliishia darasa la nne.

“Kama mtu umeelewa kitu kinachofundishwa kuna faida fulani, kwa nini mimi ninakamatwa? Mimi nimeishia darasa la nne nikagundua ndani ya elimu kuna faida fulani…Kwa nini mzazi wangu na mimi tukamatwe kurudishwa shuleni? Tuendelee miaka 20 isiyokuwa na faida?,” alihoji.

Akizungumzia watoto wanaowatelekeza wazazi wao baada ya kupata kazi, Kishimba alitoa wito kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto, kupeleka muswada bungeni utakaomwezesha mzazi kumshtaki mtoto ambaye anakataa kumpatia fedha wala kupokea simu yake.

“Unakuta wazee kijijini wanahangaika na Tasaf (mpango wa kunusuru kaya masikini) lakini mtoto ana maisha mazuri Dar es Salaam kila siku anafanya bethidei,” alisema.

Alihoji mbona Serikali mwanafunzi anapofikisha kidato cha sita humpatia mkopo wenye riba anaolazimika kuulipa akianza kazi.

“Mimi nina kosa gani kumdai mwanangu? Kwanini wazazi tujiandae kulalamika na kutoa radhi? Kwanini Serikali isitusaidie? Mwanasheria Mkuu wa Serikali uko hapa,” alisema.

“Mwanangu nimemtunza, nimemsomesha kwa nini nijiandae kuja kutoa radhi? Anatakiwa kunisaidia. Niruhusiwe kama hakutoa fedha hakupokea simu, mimi niende polisi nikamshtaki,” alisema Kishimba.

Chanzo: mwananchi.co.tz