MBUNGE wa Handeni Mjini, Reuben Kwagilwa, amesema kuanzisha wiki hii ataanza kuzishughulikia changamoto tatu ambazo kwa muda mrefu zimekuwa ni matatizo sugu kwa wananchi wa jimbo hilo.
Akizungumza na HabariLEO juzi, Kwagilwa alizitaja changamoto hizo kuwa ni upatikanaji wa maji kwa baadhi ya maeneo, migogoro ya ardhi na tatizo la kukatika kwa umeme.
Kuhusu migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Handeni, alisema imegawanyika katika sehemu mbalimbali ambazo ni migogoro ya mipaka baina ya kata na kata, mgogoro wa mpaka baina ya wilaya ya Handeni na Kilindi, migogoro ya ardhi baina ya watu na watu na migogoro ya ardhi baina ya watu na taasisi.
Alisema katika kutatua changamoto hiyo, Halmashauri ya Mji wa Handeni imetenga ofisi itakayotumika kama mahakama ya ardhi na kwamba wanachosubiri ni kumwomba waziri mwenye dhamana ya ardhi awaletee hakimu kushughulikia masuala ya ardhi.
"Tunachosubiri ni kumuomba waziri wa ardhi kutuletea hakimu kwa sababu huduma za kisheria za migogoro ya ardhi wananchi wa Handeni wanazifuata Korogwe ambapo ni mbali," alisema.
Kuhusu changamoto ya umeme, alisema tayari ameshauandikia barua Uongozi wa Shirika la Umeme la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) wilayani Handeni ili wakutanekujadili suala hilo ili ikibidi, baadaye alifikishe bungeni kwa ufumbuzi zaidi.
Akizungumzia upatikanaji wa huduma za maji, alisema mradi wa kwanza wa kutoa maji Korogwe kupeleka Handeni (HTM) unahudumia mitaa 30 kati ya mitaa 60 katika kata 12 za jimbo hilo na kwamba, wanategemea mradi mkubwa wa HTM mpya ambapo serikali imetoa Sh bilioni 380 utaondoa changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, wanategemea serikali kujenga upya bwawa la maji la Kenkambala katika Kata ya Kwediyamba lilisombwa na maji kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mwezi Oktoba mwaka jana sambamba na kuchimba visima virefu katika maeneo ambayo hayatapata huduma za maji za HTM na bwawa hilo.