Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge Chadema asaka fursa kukutana na JPM

Sat, 29 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mbunge wa Arumeru Magharibi (Chadema), mkoani Arusha, Gibson Ole Meseyeki  anatafuta fursa kukutana na Rais John Magufuli ili kumweleza juu ya kero za jimbo lake, baada ya kudai kutengwa siku Rais Magufuli alipotembelea jimbo hilo na kuzindua mradi wa maji.

Desemba 2, 2018, Rais Magufuli alifanya ziara katika jimbo hilo, kuzindua mradi wa maji utakaogharimu kiasi cha Sh520 bilioni na pamoja na mengine alieleza kusikitishwa na kutoonekana mbunge wa jimbo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Kimnyaki.

Akizungumza  na Mwananchi jana Ijumaa Desemba 28, 2018 juu ya mikakati yake ya mwaka 2019 baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu, Meseyeki alisema anatafuta fursa ya kukutana na Rais Magufuli na kumwomba wilaya mpya kwani sasa kuna tatizo kutokana na wilaya hiyo yenye halmashauri mbili kuwa na kero nyingi.

“Siku ile Rais alipokuja kwenye jimbo langu, sikupewa taarifa nilikuwa Dar es Salaam, lakini kuna mambo walizungumza pale wabunge wa majimbo mengine nadhani si kilio sahihi cha wananchi wa Arumeru,” alisema.

Meseyeki alisema katika jimbo hilo, kuna tatizo la kiutendaji kutokana na kuwa na halmashauri mbili ya Arumeru na Arusha Dc hivyo kuhitaji wilaya lakini kuna tatizo la kutotatuliwa migogoro ya ardhi, hospitali ya wilaya haina vifaa na kuna barabara nyingi muhimu ambazo zinapaswa kutengenezwa.

“Ningepata fursa ya kuzungumza pale ningezisema hizi kero na ndio sababu bado natafuta fursa ya kukutana na Rais ili kumweleza kero hizi ambazo baadhi zinachangiwa na viongozi wa Serikali,” alisema.

Mbunge huyo, hata hivyo alikanusha uvumi wa muda mrefu kuwa alikuwa na mpango wa kujiunga na CCM na kueleza ataendelea kuwa Chadema kwani bado anaamini chama hicho ni imara na kinaweza kutatua kero za wananchi.

“Mimi bado naamini katika Chadema kuwa tunaweza kuendelea kusaidia wananchi na hivyo sina mpango wala nia ya kuhama sasa hata mwaka 2020 na chama changu kikinipa fursa nitagombea tena,” alisema.

Alisema licha ya ukimya wake lakini mambo yote aliyowaahidi wananchi wakati wa kampeni zake, anaendelea kutekeleza kwa kushirikiana na Serikali na  wadau wengine.

“Tumefikia, hatua, nzuri ahadi zinatekelezwa shida ya maji inafanyiwa kazi lakini barabara zinatengenezwa na mimi kama mbunge nina kazi ya kufuatilia utekelezwaji wa maagizo ya Serikali,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuna miradi ambayo inaendelea kutekelezwa kama ujenzi wa shule ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanapata nafasi.



Chanzo: mwananchi.co.tz