Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge Chadema apewa siku 7 maboksi ya kura

Dfc629e81b08335de5d38a326438ef2a Mbunge Chadema apewa siku 7 maboksi ya kura

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

BUNGE limemtaka Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Felister Njau, awasilishe ushahidi ndani ya siku saba kuhusu mabegi matano ya kura feki anayodai aliyaona siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka jana katika Jimbo la Kawe, Dar es Salaam.

Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, alitoa uamuzi huo jana bungeni kwa kusema, kwa mujibu wa kifungu cha kanuni namba 70 za Bunge , kwa kuwa mbunge huyo

amekataa kufuta kauli yake kwa kudai ana ushahidi wa mabegi hayo anapaswa kuwasilisha ushahidi kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge kabla ya Jumatano ijayo.

Alisema Kamati ya Maadili itatoa taarifa kwake kuhusu uamuzi wa jambo hilo na kwamba, unatakiwa utolewe kabla ya kuahirishwa mkutano wa Bunge Ijumaa Februari 12 mwaka huu.

"Mbunge utatakiwa kupeleka ushahidi kwenye Kamati ya Maadili hadi Jumatano ijayo, ili kamati ikae ili kabla ya Bunge kwisha tutoe uamuzi," alisema Dk Tulia.

Kabla ya uamuzi huo, Dk Tulia alimtaka Njau afute kauli yake ili kuiondoa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge, lakini mbunge huyo alikataa kufuta na kudai akitakiwa kuleta ushahidi ataleta.

Naibu Spika Dk Tulia alitoa nafasi mara mbili kwa mujibu wa kifungu namba 71 cha Kanuni za Bunge akimtaka Njau aondoe kauli yake kama hana ushahidi lakini Mbunge huyo aliendelea na msimamo wake kwamba ana ushahidi kwamba aliyaona makasha hayo.

Mbunge Njau aliendelea na msimamo huo hata baada ya Mbunge wa Jimbo la Kawe, Josephat Gwajima (CCM) kusema alishinda kihahali kwa kupata kura 100,094 na kwamba akimshinda mgombea kwa tiketi ya Chadema, Halima Mdee aliyepata kura 30,000.

Mbunge Njau alidai kuwa, alikuwa meneja wa kampeni wa Halima Mdee.

Alisema bungeni kuwa, pamoja na msisitizo kuhusu demokrasia nchini kama ilivyoandikwa kwenye hotuba ya Rais John Magufuli ya kuzindua Bunge katika ukurasa wa 72 kwamba ataendelea kulinda demokrasia, haki na vyombo vya habari, inatakiwa kutekelezwa kwa vitendo.

Dk Tulia aliwahimiza wabunge ambao zaidi ya asilimia 60 ni wapya wazisome kanuni za Bunge ili wazielewe vizuri.

Bunge la 12 jana liliendelea kujadili hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati akilizindua mwishoni mwa mwaka jana.

Chanzo: habarileo.co.tz