Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge Chadema ‘aliyetajwa’ kuhamia CCM avunja ukimya

33621 Mbunge+pic.png Tanzania Web Photo

Thu, 27 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Jaffar Michael ni miongoni mwa wabunge ambao wamekuwa wakidaiwa kuwa na mpango wa kuhamia CCM, lakini jana amefunguka kuhusu ukimya wake wa muda mrefu, akitaka aendelee kuaminiwa na wapigakura wake.

Kwa muda mrefu sasa, amekuwa hasikiki kama ilivyokuwa imezoeleka hadi kuzushiwa kuwa ni miongoni mwa wabunge waliokuwa katika mpango wa kuhamia CCM kama ilivyokuwa kwa wengine saba wa Chadema waliohamia chama tawala na kupitishwa kuwania tena nafasi hiyo katika majimbo yao na kuibuka washindi.

Wabunge hao na majimbo yao katika mabano ni, Dk Godwin Mollel (Siha), Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli), Ryoba Marwa (Serengeti), Joseph Mkundi (Ukerewe), James Ole Millya (Simanjiro), Pauline Gekul (Babati Mjini).

Abdallah Mtulia (Kinondoni), Zuberi Kuchauka (Liwale) na Abdallah Mtolea (Temeke) walikuwa wabunge wa CUF kabla ya kuhamia CCM huku Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini) akitoka CCM na kuhamia Chadema. Hata hivyo hakugombea tena kiti hicho.

Jana katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wapigakura wake, Michael aliwataka waendelee kumwamini akiahidi kuwatumikia kulingana na hali ya kisiasa iliyopo.

Katika salamu hizo, mbunge huyo alitaja mambo sita atakayopigania mwaka 2019 kuwa ni pamoja na ujenzi wa stendi mpya ya kisasa Afrika Mashariki na Kati itakayojengwa Ngangamfumuni.

Pia, alisema atapigania kukarabatiwa kwa Uwanja wa Ndege wa Moshi, ili watalii wanaokuja kwa ajili ya kupanda Mlima Kilimanjaro waweze kutua katika uwanja huo na kuongeza biashara ya utalii. Jingine ni kuhakikisha Manispaa ya Moshi inarudi katika nafasi yake ya kwanza kitaifa katika usafi na tayari imenunua magari mapya matatu ya kusoma taka.

Michael ambaye alishika wadhifa huo mwaka 2015 akimrithi Philemon Ndesamburo ambaye sasa ni marehemu, alisema mkakati mwingine ni kuhakikisha dampo la kisasa linajengwa katika Kijiji cha Mtakuja. Alisema atahakikisha kiwanda cha kuchakata takataka kinajengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani ili kutoa mbolea kwa ajili ya kilimo. Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya, alisema magari hayo ya taka yamegharimu Sh615 milioni na kwamba kiwanda cha kuchakata taka ngumu kitafadhiliwa na Mji wa Tubingen wa Ujerumani ambao ni mji dada na Manispaa ya Moshi na umekubali kutoa Sh900 milioni. Kuhusu ujenzi wa stendi mpya ya Ngangamfumuni, alisema utagharimu karibu Sh27 bilioni na tayari mkandarasi amepatikana na ujenzi utaanza mwanzoni mwa mwaka ujao.



Chanzo: mwananchi.co.tz