Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge Chadema afananisha wanaohama vyama na kenge kwenye msafara wa mamba

10277 Msigwa+pic

Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema katika msafara wa mamba, kenge wapo, akifananisha msemo huo wa wanachama wa vyama vya upinzani wanaohamia CCM.

Amesema katika harakati za kuleta mabadiliko si jambo la ajabu wakatokea wasaliti, kubainisha kuwa wasaliti hao ni waliokuwa viongozi na wanachama wa Chadema na vyama vingine vya upinzani waliohamia chama tawala.

Mchungaji Msigwa ametoa kauli hiyo leo jioni Jumapili Agosti 5, 2018 katika kipindi cha Siasa za Kanda kinachorushwa na kituo cha televisheni cha KTN cha nchini Kenya.

Mada kuu katika kipindi hicho ilikuwa ni kujadili hali ya siasa za upinzani barani Afrika huku wachangiaji wa mada hiyo wakiunganishwa kutoka Zambia, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Zimbabwe, Kenya, Uganda na Tanzania.

Mchungaji Msigwa ametoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na mtangazajii anaonaje hali ya Chadema katika kujiimarisha katikati ya mazingira ya viongozi na wanachama wake kuhamia CCM.

Katika ufafanuzi wake Mchungaji Msigwa amesema licha ya kuwa kuhama chama ni haki ya msingi, wengi wanachukua uamuzi huo kwa kushawishiwa kwa ahadi mbalimbali.

“Kama wangekuwa wanachukuliwa na kufanya kazi ya chama mimi sioni tatizo lakini wanaahidiwa nafasi za uongozi, hii si sawa kabisa. Hii inaua mawazo pinzani,” amesema.

mbunge huyo wa Iringa Mjini amekiri changamoto hiyo ya wanachama kuhama haipo Tanzania pekee bali kwa vyama vingi vya upinzani barani Afrika, kubainisha kuwa Chadema wanaongeza mbinu za kujenga imani na itikadi kwa wanachama wao.

Akichangia mada hiyo, Profesa Fulbert Namwanga raia wa Kenya anayefundisha nchini Marekani amesema demokrasia katika nchi nyingi za Afrika haijakomaa.

“Demokrasi si pevu ina ufisadi mwingi, baadhi hawaelewi maana ya demokrasia na hawaelewi maana ya upinzani wanauona kama uadui. Ni kawaida wapinzani kununuliwa, ni jambo la kuhuzunisha sana,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz