Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge CCM ataka kujua kwa nini Serikali haiitaki PPP

57201 Pic+serukamba.png

Tue, 14 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba ameitaka Serikali ya Tanzania kueleza kwa nini miradi mingi inatekelezwa na Serikali yenyewe bila kushirikisha ushirikiano baina ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP).

Serukamba ametoa hoja hiyo leo Jumatatu Mei 13, 2019 wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka 2019/20 ya Sh4.9 trilioni.

Mbunge huyo amesema amesoma kitabu chote cha hotuba cha wizara hiyo, “Sijaona popote tunaongelea barabara au mradi wowote wa PPP.”

Serukamba amesema kunahitajika kuwatofautisha marais waliopita na Rais wa sasa John Magufuli.

Amesema hayati baba wa Taifa, Julius Nyerere, marais Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wote walijenga barabara, “Lakini tunahitaji kumtofautisha Rais Magufuli na marais waliopita .

Serukamba amesema kumtofautisha huko kutawezekana iwapo Serikali itakubali kujenga barabara za ‘super highway’, “Ila wapo watu serikalini wanasema kwa kujenga SGR (reli ya kisasa) barabara hatuna kazi nazo.”

Habari zinazohusiana na hii

“Reli hiyo inayojengwa hata ikiisha, reli kazi yake ni mizigo, tujenge barabara, duniani wanajenga barabara kwa kushirikiana na PPP. Namna bora ya kumfanya (Rais Magufuli) kuwa tofauti na wengine ni tujenge barabara kwa kushirikiana na PPP,” amesema.

Akiendelea kuchangia, Serukamba amesema barabara ya “Chalinze tumeiondoa, ukiwauliza serikalini unaambiwa tumeiondoa kwa sababu ya SGR.”

“Haiwezekani kilomita 100 tunakwenda masaa nane, lazima tufanye vitu kama kusafirisha mizigo mapema, sielewi kwa nini Serikali haitaki miradi ya PPP,” amesema.

Amesema mataifa mbalimbali duniani yamekuwa yakitekeleza miradi mbalimbali kwa kushirikiana PPP jambo ambalo kwa sasa halifanyiki nchini hivyo miradi mingi kuchukua muda mrefu kuitekeleza.

“Tunataka kufanya yote, ili twende kwa kasi tuwaachie wengine wafanye, sielewi kwa nini Serikali haitaki miradi ya PPP,” amerudia huku akishangiliwa na wabunge wa pande zote.

Serukamba amegusia pia suala la viwanja vya ndege kujengwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) akisema suala hilo lirejeshwe Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kwani Tanroads wana shughuli kubwa ya kufanya kama ujenzi wa madaraja na barabara.

Amesema TAA iachiwe jukumu la viwanja vya ndege ili kurejesha ufanisi mkubwa wa suala hilo.

Serukamba ameungwa mkono na Mbunge wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge ambaye amesema, “Sekta binafsi ishirikiane na sekta ya umma, katika hili tutaharakisha maendeleo haya.”

Chenge aliyewahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali amesema, “Reli yetu ya kati tunayojenga sasa, ni afadhali tukachukua mikopo ya muda mrefu kuliko hii ya masharti nafuu itakuja kutuumiza hata kabla hatujamaliza.”

Mbobezi huyo wa sheria nchini amegusia pia suala la kuunganisha mikoa yote kwa lami akisema, “Sisi Simiyu hatujaunganishwa na mikoa ya Singida na Arusha sijajua kwa nini.”

Mjadala wa bajeti hii ulioanza Mei 9, 2019 utahitimishwa leo jioni Jumatatu kwa mawaziri kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge.

Chanzo: mwananchi.co.tz