Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge CCM aibua sakata la Richmond kwenye kampeni Monduli

16433 Pic+mbunge TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Monduli. Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga amewataka wakazi wa Monduli mkoani Arusha kumuuliza waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa sababu za kujiuzulu baada ya kuibuka kwa kashfa ya Richmond.

Mlinga alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kampeni Jimbo la Monduli uliofanyika eneo la Makuyuni.

Alisema Lowassa anamshambulia mgombea wa CCM katika jimbo hilo, Julius Kalanga kuwa amejiuzulu uanachama wa Chadema na kuhamia chama tawala kwa sababu alikuwa na deni la Sh600 milioni, wakati yeye alijiuzulu uwaziri mkuu kwa tuhuma fedha za Richmond.

Waziri huyo mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, amekuwa hazungumzii sakata hilo na inapotokea kulizungumzia amekuwa akieleza kuwa alijiuzulu kwa misingi ya uwajibikaji ili kuilinda Serikali ya CCM na kwamba ushiriki wake ulitokana na maagizo kutoka juu.

Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Lowassa alikwepa kuzungumzia sakata hilo, ambapo katika mkutano wa kampeni kijiji cha Mvumi wilayani Chamwino mkoani Dodoma uliofanyika Septemba 11, 2015 alikataa kujibu swali lililomtaka aeleze kilichotokea kwenye sakata hilo akisema, “swali hilo halina maana”.

Lowassa ambaye siku hiyo aliamua kutohutubia na badala yake kuruhusu wananchi wamuulize maswali, aliulizwa swali hilo na Michael Makanyi aliyetaka kujua kama mwanasiasa huyo aliyegombea urais kwa tiketi ya Chadema anahusika kuipa Richmond ya Marekani zabuni ya kufua umeme wa dharura.

Richmond ilipewa zabuni hiyo wakati nchi ilipokumbwa na tatizo la nishati hiyo mwaka 2006. Lowassa alijiuzulu mwaka 2008 na Rais Jakaya Kikwete kumteua Mizengo Pinda kuwa waziri mkuu.

Alichosema Mlinga

Katika mkutano huo wa kampene jana, mbunge Mlinga aliwauliza wananchi, “jamani kati ya anayedaiwa na ambaye amejiuzulu kwa tuhuma za kuchukua fedha za umma nani bora?”

Alisema watu wengi wamekopa katika taasisi mbalimbali za fedha na wanadaiwa, lakini si tatizo kwa kuwa anayekopa hulipa na kwamba deni halimfungi mtu.

Aliwataka wakazi wa Monduli kupuuza tuhuma kuwa Kalanga alijiuzulu ili kulipiwa deni kwani kauli hizo ni za kisiasa.

Mbowe aahidi ushindi

Kutoka Hai mkoani Kilimanjaro, katika uzinduzi wa kampeni za Chadema kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kia, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema ana uhakika atashinda vita dhidi ya CCM akidai chama hicho tawala kinawarubuni madiwani wa chama chake kujiuzulu na kuhama.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Yohana Laizer kwa tiketi ya Chadema kujiuzulu na kujiunga na CCM, na baadaye kuteuliwa kuwania tena udiwani wa kata hiyo.

“Haya mambo ni ya ajabu sana. Magari yanatembea na vijana wanateka watu usiku na mchana na kuwalazimisha kuhama Chadema wakikataa wanawabambikia kesi,” alisema Mbowe akiituhumu CCM kukifanyia mchezo mchafu chama chake.

Nyongeza na Daniel Mjema

Chanzo: mwananchi.co.tz