Dodoma. Mbunge wa Maswa Magharibi (CCM) nchini Tanzania, Mashimba Ndaki amesema kuna tatizo la transfoma zinazofungwa na wakandarasi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambazo zimekuwa zikiharibika haraka.
“Je Serikali inachukua hatua gani juu ya kuondoa tatizo hili,” amehoji Ndaki wakati akiuliza swali la bungeni leo Ijumaa Novemba 15, 2019.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na REA imekuwa ikibaini baadhi ya transfoma kuharibika muda mfupi baada ya kufungwa katika baadhi ya maeneo ya miradi ya umeme vijijini inayofadhiliwa na Mfuko wa Nishati Vijijini (REF).
Aidha amesema uchunguzi uliofanyika umeonyesha katika baadhi ya maeneo transfoma zilizofungwa ziliharibika kutokana na uwepo wa radi katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu ikiwamo mikoa ya Kagera, Katavi na Njombe.
“Kutokana na hali hiyo, baadhi ya vifaa vya kulinda transfoma kuathirika na radi hushindwa kufanya kazi vizuri na hivyo kusababisha transfoma kuharibika zinapopigwa na radi,” amesema.
Aidha, Subira amesema matukio ya wizi wa baadhi ya vifaa (earth rods) na waya za shaba zinazotumika katika mfumo wa ulinzi wa transfoma yamesababisha transfoma hizo kuungua.
Amesema baadhi ya transfoma hasa za kutoka nje ya nchi zimekuwa hazina ubora kutokana na hali hiyo Serikali imechukua hatua ya kuhakikisha transfoma zote zinazotumika kusambaza umeme zinatokana na viwanda vya hapa nchini vilivyothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Hata hivyo, amesema elimu kwa wananchi imeendelea kutolewa kwa ajili ya ulinzi wa miundombinu ya umeme ikiwamo transfoma katika maeneo yao ya miradi