Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge CCM adai Dar inaongoza kwa watoto wa mitaani, Serikali yamjibu

94717 Watoto+pic Mbunge CCM adai Dar inaongoza kwa watoto wa mitaani, Serikali yamjibu

Thu, 6 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge Viti Maalum (CCM) Fakharia Shomary Khamis amedai kuna ongezeko kubwa la watoto wa mitaani jijini Dar es Salaam, kwamba wengi wanakosa haki zao.

Ameeleza hayo leo Alhamisi Februari 6, 2020 bungeni mjini Dodoma wakati akiuliza swali la msingi bungeni kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania kukabiliana na tatizo la watoto wa mitaani.

Akijibu swali hilo, naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema watoto 6,393 kutoka mikoa sita nchini wanaoishi na kufanya kazi mitaani wametambuliwa.

Ametaja mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Arusha, na Iringa.

Amesema idadi hiyo watoto wa kiume ni 4,865 na wa kike 1,528 na walikuwa wakiishi mitaani kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kufiwa na wazazi, migogoro ya familia, kutengana kwa wazazi, vitendo vya unyanyasaji na ukatili na umasikini katika ngazi ya kaya.

Amesema wizara hiyo ilifanya utafiti watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani Mei 2018 na kwamba utafiti huo ulihusisha mikoa sita nchini.

Pia Soma

Advertisement
“Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Arusha na Iringa na jumla ya watoto 6,393, kiume 4,865 na wa kike 1,528 wanaishi na kufanya kazi mitaani walitambuliwa,” amesema.

Dk Ndungulile amesema katika kipindi cha Oktoba 2018 hadi Machi 2019, watoto 2,702 walipatiwa huduma mbalimbali.

Amefafanua kuwa Mkoa wa Arusha watoto (330), Dar es Salaam (475), Dodoma (337), Iringa (313), Mwanza (770) na Mbeya (447).

"Huduma zilizotolewa ni pamoja na huduma za afya, chakula, malazi, kurudishwa shuleni, stadi za ufundi, stadi za maisha, kuunganishwa na familia pamoja na msaada wa kisaikolojia na kijamii,” amesema.

Dk Ndugulile amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa malezi na ulinzi wa watoto wakiwemo walio katika mazingira hatarishi.

"Pia itaendelea kuwajengea uwezo wazazi na walezi kwenye eneo la stadi za malezi na ulinzi wa watoto,” amesema.

Ametoa rai kwa jamii kuhakikisha jukumu la matunzo, malezi na ulinzi wa mtoto linatekelezwa ipasavyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz