Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe, wabunge Chadema wakalia kuti kavu

101584 Pic+mbowe Mbowe, wabunge Chadema wakalia kuti kavu

Thu, 14 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

BUNGE limeweka masharti mawili kwa wabunge 15 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliotii agizo la chama chao la kuwataka kutohudhuria bungeni kwa siku 14 ili kujitenga na kuangalia afya zao kipindi hiki cha janga la corona.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Spika jana, wabunge hao ni watoro kwa kuwa hawajahudhuria vikao vya Bunge kwa wiki mbili sasa.

Masharti yaliyotangazwa na Ofisi ya Spika ni pamoja na kurejea bungeni au kurudisha fedha walizolipwa mara moja. Pia wanatakiwa kuwasilisha ushahidi kwamba wamepimwa na hawana maambukizo ya corona kabla ya kuruhusiwa kuingia bungeni.

Taarifa hiyo ilikuwa na majina ya wabunge hao kuwa ni pamoja na Freeman Mbowe, Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni; Mnadhimu wa Kambi hiyo na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya; na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu'; Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga; na Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule 'Profesa Jay'.

Wengine ni wabunge wa Viti Maalum, Catherine Ruge; Devotha Minja; Joyce Mukya; Aida Khenan; Upendo Peneza; Rhoda Kunchela na Grace Kiwelu.

Katika hiyo, ilielezwa kuwa Spika Job Ndugai ameagiza Kitengo cha Usalama cha Bunge kutoruhusu wabunge hao kuingia kwenye maeneo ya Bunge kuanzia Mei 13 mwaka huu (jana) mpaka watakapotimiza masharti hayo.

“Baadhi ya wabunge wa Chadema wamekuwa watoro kwa kutohudhuria vikao vya Bunge bila ruhusa ya Spika kwa muda wa wiki mbili kinyume cha masharti ya Kanuni ya 146 inayosisitiza wajibu wa kila mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Ilibainishwa zaidi katika taarifa hiyo kuwa wabunge hao walisusia vikao huku wakiwa wamelipwa posho ya kujikimu ya kuanzia Mei Mosi hadi Mei 7 mwaka huu kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya Tano ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Mei Mosi, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mbowe, alitangaza uamuzi wa chama hicho kuwataka wabunge wao kutohudhuria vikao vya Bunge na kamati kwa siku 14, lakini baadhi ya wabunge wa chama walionekana kukaidi agizo hilo kwa kuhudhuria bungeni.

Mei 11, Chadema ilitangaza kuwafukuza uanachama wabunge wanne huku mmoja akivuliwa nyadhifa zote za ndani ya chama na kuwataka tisa kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo, Spika Ndugai aliwataka wabunge hao kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa atawalinda huku akiwataka kuendelea kuhudhuria vikao vya Bunge.

Pia, itakumbukwa kuwa Mei 5 mwaka huu, Spika Ndugai aliwataka wabunge hao kurejea bungeni na iwapo hawatafanya hivyo, warejeshe Sh. milioni 110.1 walizolipwa kwa ajili ya kujikimu.

Spika alikwenda mbali zaidi na kutaja kiwango cha fedha kwa kila mbunge aliyelipwa na kwamba wasipofanya hivyo, hatua zitachukuliwa huku akitishia kutowalipa mishahara yao ya mwezi huu.

Tamko jipya la Ofisi ya Spika limetoka ikiwa imebaki siku moja kwa wabunge hao kurejea bungeni kwa kuwa leo wanamaliza karantini waliyotakiwa kuifanya tangu Mei Mosi mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live