Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe kula Krismasi, Mwaka Mpya mahabusu mara ya pili

Mbowe 0 (1) Mbowe kula Krismasi, Mwaka Mpya mahabusu mara ya pili

Mon, 20 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu imeahirisha hadi Januari 10, 2022 usikilizwaji wa kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu kwa mapumziko ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Kwa uamuzi huo, Mbowe na wenzake watasherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya akiwa mahabusu kwa mara ya pili ndani ya miaka mitatu.

Mara ya kwanza, Mbowe alisherehekea sikukuu hizo akiwa mahabusu mwaka 2018 hadi mwaka 2019 baada ya kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu katika kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili na wenzake wanane, wakiwemo viongozi wengine wa juu wa Chadema na wabunge.

Mbowe na aliyekuwa mbunge wa Tarime mjini, Ester Matiko walifutiwa dhamana baada ya kushindwa kuhuduria kesi hiyo mara kadhaa.

Hata hivyo, walikata rufaa Mahakama ya Kuu ambayo Machi Mosi, 2019 iliwarejeshea dhama yao baada ya kutengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu.

Jana, Mahakama Kuu (Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi) iliiahirisha kesi dhidi yao baada ya kumaliza kusikiliza pande zote zilizovutana vikali kufuatia ombi la Jamhuri kutaka mahakama ipokee Sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na vifaa vingine vilivyodaiwa kukutwa nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza, Halfan Bwire Hassanj. Mawakili wa utetezi walipinga vikali hatua hiyo wakidai kuwa uwasilishwaji wa vifaa hivyo mahakamani haukufuata sheria.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya, ambao pamoja na Bwire walikuwa askari wa JWTZ Kikosi cha Makomando kabla ya kuachishwa kwa sababu za kinidhamu.

Wote wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama kutenda vitendo vya kigaidi, kushiriki vikao na kufadhili vitendo vya kigaidi kama vile kulipua vituo vya mafuta na maeneo ya mikusanyiko ya watu, kuhamasisha maandamano yasiyokoma, kuzuia barabara kwa magogo na kumjeruhi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofautitofauti Agosti, 2020 katika mikoa Kilimanjaro, Morogoro na Dar es Salaam.  

Chanzo: www.tanzaniaweb.live