Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe kufanya ziara ya siku saba Uingereza

IMG 4340 Mbowe.jpeg Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza katika moja ya tukio la chama hicho

Sun, 18 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kesho Juni 19, 2023 ataanza ziara ya kikazi ya siku saba nchini Uingereza zikiwa zimepita wiki mbili tangu alipofanya ziara kama hiyo katika nchi za Italia na Ujerumani.

Ziara hiyo ya Mbowe ni ya pili ndani ya mwezi huu (Juni) pekee ambapo ziara ya kwanza aliifanya Juni 5, 2023 katika nchi hizo akiwa pamoja na viongozi wenzake wa Chadema, Makamu Mwenyekiti (Bara), Tundu Lissu na Katibu Mkuu, John Mnyika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika (DUA), anatarajiwa kuondoka nchini kesho Juni 19, 2023 alfajiri kuelekea nchini Uingereza.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba, akiwa nchini Uingereza, Mbowe atahudhuria maadhimisho ya miaka 40 tangu kuasisiwa kwa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU) yanayofanyika kwa siku mbili; Juni 19 na 20, 2023 jijini London.

Chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu mstaafu wa Canada, Stephen Harper, ufunguzi wa maadhimisho haya unahudhuriwa na viongozi wanachama wa IDU vikiwemo vyama tawala na vya upinzani kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni.

Ufunguzi wa maadhimisho hayo utafanywa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Boris Johnson miongoni mwa watakaohudhuria mkutano huo ni viongozi wakuu wa vyama hivyo wakiwemo Marais, mawaziri wakuu, wabunge, mawaziri walioko madarakani na wastaafu.

Mrema anaeleza katika taarifa yake kwamba akiwa nchini humo, Mbowe atashiriki kikao cha uongozi wa IDU Juni 21, 2023 ambakp yeye pamoja na mwenyekiti mwenza wa DUA watawasilisha taarifa juu ya hali ya demokrasia barani Afrika na uimarishwaji wa DUA.

Pia, amebainisha kwamba Mbowe atashiriki kama mgeni maalumu kwenye mjadala utakaoangazia mwenendo wa kisiasa na mahitaji ya mabadiliko muhimu yatakayoimarisha amani na umoja nchini Tanzania ulioandaliwa na Chatham House.

Taarifa hiyo inabainisha kwamba ratiba ya Mbowe inahusisha pia vikao na mazungumzo na viongozi na mashirika mbalimbali ya maendeleo na demokrasia.

Mrema amesema Mbowe anatarajiwa kuhitimisha ziara yake kwa kuzungumza na Watanzania waishio Uingereza kwenye mkutano utakaofanyika Juni 24, 2023 jijini London kabla ya kurejea nchini Juni 25, 2023.

Chanzo: Mwananchi