Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe kuchukuliwa fomu ya uenyekiti kesho

85708 Pic+mbowe Mbowe kuchukuliwa fomu ya uenyekiti kesho

Sun, 24 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anatarajiwa kuchukuliwa fomu kesho na vijana waliojitolea kumchangia ili kutetea nafasi hiyo.

Novemba 21,2019 baadhi ya makundi likiwemo la vijana na uongozi wa jimbo la Segerea walieleza sababu za kumchukulia fomu Mbowe ili kutetea nafasi hiyo.

Akizungumza na MCL Digital leo Novemba 24,2019 mratibu wa vijana katika mpango huo, Twaha Mwapaya amesema zoezi la ukusanyaji fedha limekamilika na kesho Jumatatu watamchukulia fomu.

"Kwa mimi binafsi tayari nimekusanya laki nane na gharama ya fomu ni milioni moja, tumegawana makundi tofauti katika mchakato wa ukusanyaji fedha," amesema Mwapaya

Amesema kikao cha mwisho kwa ajili ya kukamilisha mrejesho kitafanyika leo ambapo kila kundi lililopewa jukumu litawasilisha mrejesho pamoja na fedha zilizokusanywa.

"Kesho Jumatatu tutamchukulia Mbowe fomu na kumpelekea popote atakapokuwepo kwa ajili ya kumkabidhi, tunaamini yeye ndiye atakayetuvusha katika kipindi hiki ambacho demokrasia imekandamizwa," amesema.

Ameongeza kuwa endapo makusanyo yatazidi lengo fedha zitakazobaki zitamsaidia kwenye kampeni ikiwa ni pamoja na kuwafikia wajumbe walioko mkoani.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi iliyotangazwa na katibu mkuu wa chama hicho Dk Vincent Mashinji, mkutano mkuu wa chama hicho unatarajiwa kufanyika Desemba 18, 2019 ambapo pia uchaguzi wa viongozi ngazi ya Taifa utafanyika.

Chanzo: mwananchi.co.tz