Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe amelipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kusimamia mikutano ya hadhara kwa amani na haki tangu iliporuhusiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema kwa sasa mabomu ya machozi yamesahaulika kwa kuwa jeshi hilo linatenda kazi za msingi za kulinda haki, amani na mali za watanzania. Mbowe alisema katika ufunguzi wa mikutano ya hadhara kanda ya Nyasa uliofanyika katika viwanja vya Ruanda, Nzovwe Jijini Mbeya.
“Watu wana furaha, na Mbeya leo tunaondoka kwa furaha, huko tulikotoka huji kwenye mkutano wa hadhara bila kuona lori la washawasha limesimama kule, tumezungumza na Rais(Samia) kwenye vikao vya maridhiano tukasema namna hii ya kupora uhuru wa wananchi lazima ikome,” alisema.