Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe ataka Watanzania walaani chaguzi ndogo

16625 Pic+mbowe TanzaniaWeb

Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hai. Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, amewataka Watanzania bila kujali itikadi za vyama vyao, kulaani chaguzi ndogo zinazoendelea nchini kutokana na wabunge na madiwani kujiuzulu.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB) na mbunge wa Hai, alidai uchaguzi mdogo wa ubunge pekee, unagharimu kati ya Sh1.5 bilioni na Sh2.5 bilioni.

Kuhusu gharama za chaguzi ndogo za udiwani, Mbowe alidai hugharimu kati ya Sh250 milioni na Sh500 milioni, na kudai hayo ni matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi na yanapaswa kulaaniwa.

Mbowe alitoa madai hayo juzi katika viwanja vya Mtakuja katika Kata ya Kia, wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, ambapo Chadema kimemsimamisha Hassan Kibuo.

“Inaonekana sasa ni usaliti na ni makosa kujiunga na chama kingine cha siasa nje ya CCM. Uchaguzi wa marudio wa diwani unagharimu taifa letu kati ya Sh250 milioni na Sh350 milioni,” alidai.

Naibu Katibu mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, aliwaomba wananchi wa kata hiyo, kutokubali kupeleka watu aliodai ni virusi katika baraza la madiwani.

“CCM wanapata tabu sana kwa nini Halmashauri zinazoongozwa na Chadema ziko vizuri katika kuwaletea wananchi maendeleo,” alidai. Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Susan Kiwanga, aliwataka wananchi kuwanyima kura wagombea wa CCM katika nafasi zote wanazogombea, ili kuwaadhibu kutokana na ugumu wa maisha wanaopitia.

Chanzo: mwananchi.co.tz