Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe asimulia alivyotoroka nchini kukimbilia Dubai

Mbowe Freeman Aikael Mbowe asimulia alivyotoroka nchini kukimbilia Dubai

Wed, 27 Mar 2024 Chanzo: Mwananchi

Kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na baadaye kushitakiwa kwa ugaidi, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesimulia namna alivyokimbilia Dubai na kurejea nchini mwaka 2021.

Mbowe alitoa simulizi hiyo juzi Machi 25,2024 wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa wananchi katika Jimbo la Hai ambalo aliwahi kuwa mbunge.

Amesema alikimbia nchi kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya wa Namanga.

Mwanasiasa huyo ni miongoni mwa viongozi wa Chadema waliokimbia nchi baada ya uchaguzi akiwamo makamu wake, Tundu Lissu aliyeishi uhamishoni Ubelgiji huku aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema akikimbilia Canada.

Mbowe alitoa simulizi hiyo ambayo alisema ni ya kwanza kuisimulia tangu kumalizika kwa uchaguzi huo mkuu wa mwaka 2020.

Alisema alitoroka Tanzania baada ya kuruhusiwa na polisi wa kituo cha Oysterbay kilichopo jijini Dar es Salaam kwenda Nairobi Kenya kwa ahadi kuwa angerudi.

Kiongozi huyo alisema alirejea nchini Aprili 2021 na akasema yaliyoendelea baada ya hapo haikuwa nafasi ya kuyaelezea, lakini inafahamika Julai 2021 alikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la ugaidi.

Alikamatwa usiku wa kuamkia Jumatano ya Julai 21,2021 akiwa katika hoteli ya Kingdom iliyoko mtaa wa Ghana Jijini Mwanza pamoja na viongozi wengine wa Chadema, lakini yeye baadaye alisafirishwa na Polisi hadi Jijini Dar es Salaam.

Mbowe alifikishwa kortini Julai 26, 2021 akishitakiwa pamoja na walinzi wake na alifutiwa mashitaka hayo na Jamhuri kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP).

Aliiondoa kesi hiyo Machi 4, 2022 akisema hana nia ya kuendelea nayo.

Januari 2023 katika mikutano mbalimbali ya hadhara aliyoifanya Kanda ya Ziwa baada ya mikutano ya hadhara kuruhusiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Mbowe aliwahi kusimulia namna alivyokamatwa jijini Mwanza hadi kushitakiwa Jijini Dar es Salaam.

Katika simulizi hizo, hajawahi kuzungumzia namna alivyofanikiwa kuondoka nchini akiwa nje kwa dhamana baada ya kuwashawishi polisi kumruhusu asafiri.

Simulizi ya Mbowe alivyokimbia nchi

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika viwanja vya Snow View katika mji wa Bomang’ombe wilayani Hai, amesema baada ya uchaguzi mkuu wa 2020 ambao hata hivyo hakupiga kura, alikwenda jijini Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo, Mbowe aliyekuwa anatetea kiti chake cha ubunge Jimbo la Hai, alishindwa kujitokeza kupiga kura kwa kile alichodai kuhofia usalama wake baada ya genge la watu wenye silaha kuvamia Hoteli ya Protea Aishi wakimsaka.

“Baada ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2020 nikaenda Dar es Salaam. Nikiwa huko nikaletewa taarifa na msamaria mwema. Hili jambo sijawahi kulisema lakini leo acha niliseme,” amesema Mbowe na kuongeza:

“Akaniambia (msiri wake) mheshimiwa Mbowe kuna kikosi kimeletwa Dar es Salaam kikushughulikie. Wanasema wewe sio mtu salama kubaki, lazima uondoke.”

“Nikachukua taarifa ile nikampelekea Siro alikuwa mkuu wa Jeshi la Polisi. Nikamwambia Simon Siro nina taarifa hizi moja, mbili, tatu ya watu wanaokusudia kuitafuta roho yangu. Siro hakunisikiliza akaniambia atanirudia.”

“Kesho yake nikamtafuta, mara tatu nne namtafuta Siro. Wakati huo tukakutana kamati Kuu Dar es Salaam tukakubaliana tuanzishe maandamano ya kulaani uchaguzi huu.”

“Siku hiyo Mbowe nikakamatwa, nikafungwa kitambaa cheusi, Nilikuwa na Lema na akakamatwa akafungwa vitamba vyeusi, tulikuwa na Meya Boniface (Jacob) wa Ubungo akakamatwa akafungwa vitambaa vyeusi. Tukatawanyishwa usiku usiku.”

“Nimepelekwa mahali nimekaa siku nne sijui niko wapi. Siku ya nne ndio nakuja kugundua kuwa niko Bagamoyo. Nimefichwa Bagamoyo. Huyu Lema huyu alipelekwa Mlandizi, Boniface alipelekwa Kibaha,”alisimulia Mbowe.

“Tulivyotoka nilijua Lema ni muoga, yaani Lema nilikuja kumshtukia yuko Nairobi ananiambia mwenyekiti niko Nairobi. Imekuwaje akasema imebidi nisepe. Nikacheka nikasema Mungu wangu,” ameelezea Mbowe huku Lema akicheka.

“Nikatolewa Bagamoyo nikarudishwa Central pale Oysterbay polisi. Nikaachiwa kwa dhamana lakini nikaambiwa ule mpango uko palepale na mimi nikaona nitakuwa mjinga. Sasa wakati huo nimeshikiliwa na polisi, niko nje kwa dhamana.”

“Nikamjengea mazingira fulani fulani hivi (ofisa polisi) kwamba niende Nairobi kidogo kwa siku mbili halafu narudi. Wakapotea kwani nilirudi! nilisepa kwa kupitia Namanga nikakaa Nairobi pale miezi miwili nikahamia Dubai.”

“Sikurudi mpaka niliposikia parapanda italia parapanda. Parapanda imelia parapanda. Nilirudi mwezi wa nne mwaka 2021 sasa hayo mengine tuyaache,” amesema Mbowe. Parapanda ni wimbo wa kikristo unaopigwa mtu akifariki dunia.

Mbowe, Lema wawasha moto

Katika mkutano huo, amezungumzia kile alichodai uwepo wa upigaji wa fedha za umma katika miradi inayotekelezwa na Serikali.

Pia katika mkutano huo amelia na kile alichodai ni gharama kubwa za kuendesha Serikali ambazo amedai kuwa zinamuumiza mwananchi wa kawaida.

Mbowe amedai kuwa gharama za kuendesha Serikali ni mzigo kwa wananchi na zinapaswa kuwa zile zenye tija.

Katika mkutano huo, amejibu hoja aliyoibua ya wabunge kuongezewa mishahara na kulipwa Sh18 milioni akisema ameona Bunge limetoa taarifa likisema yeye (Mbowe) ni muongo, akalitaka nalo liseme linawalipa kiasi gani.

“Tumesema wamepandisha mishahara ya wabunge wao wanasema Mbowe ni muongo. Wao waseme wanawalipa shilingi ngapi kwa mwezi,”alisema Mbowe.

Mbowe amesema mishahara ya wabunge haipaswi kuwa siri kama Bunge lilivyoeleza katika taarifa yao, kwa vile wabunge kama walivyo watumishi wengine wa umma, wanalipwa kwa kodi za wananchi hivyo wana haki kujua suala hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema kwa rasilimali ambazo Tanzania inazo yakiwamo madini, bahari na Hifadhi za Taifa, haikupaswa kuwa taifa la kutegemea mikopo kutoka nchi nyingine.

Lema amesema kama Serikali ingekuwa na mipango thabiti na uwepo wa utashi wa kisiasa wa kuwekeza kwenye kilimo cha mazao ya chakula na biashara, hakuna kijana ambaye angekuwa yuko mtaani kwa kukosa kazi kwa kuwa kilimo ndio kila kitu.

Chanzo: Mwananchi