Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe apigilia msumari ishu ya uraia pacha

Mbowe Pic Aomba Radhi Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe

Mon, 27 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema chama hicho iwapo kitapewa ridhaa ya kuongoza serikali kitaruhusu uraia pacha ili vijana wapate fursa ya ajira.

Akizungumza wakati anahutubia mkutano wa hadhara leo Jumapili Februari 26, 2023 wilayani Mbarali amesema sera ya CCM inasema ukiwa Mtanzania na ukapata uraia wa nchi nyingine unatakiwa ukatae uraia wa nchi yako.

“Huwezi ukawa raia wa Tanzania ukipewa uraia wa nchi nyingine lazima uukane wewe si Mtanzania ni mambo ya ajabu, niwaambie kitu kimoja nchi zote zinazounda Afrika Mashariki ni Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ndiyo wanaokataa uraia wa nchi mbili,’’amesema

Mbowe katika maelezo yake ametaja faida ya kuruhusu uraia pacha ni pamoja na wananchi wanaoishi ughaibuni kuingiza fedha za kigeni wanazotengeza kupitia ajira na taaluma mbalimbali.

“Tunawapongeza Watanzania wote waliopo mstari wa mbele kupigania uraia pacha na suala hili ni miongoni mwa sera zetu, chama chetu kinaongozwa na sera baada ya kufanya utafiti nchi inahitaji kitu gani ili tuweze kupiga hatua kimaendeleo.

“Msimamo wa chama chetu kuhusu haki ya Watanzania wanaoishi nje ni wapate uraia pacha ili kuwafungulia Watanzania fursa za ajira ili uchumi wao ukue na kuiongezea nchi fedha za kigeni,”amesema

Hoja iliyoungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama hicho Kanda ya Nyasa, Peter Msigwa aliyesema chama kimejenga utamaduni wa kuwasikiliza wananchi hivyo iwapo kitapata fursa ya kuongoza serikali basi changamoto za muda mrefu zitapatiwa ufumbuzi.

Mbowe ametoa kauli hiyo ikiwa tayari kuna shauri la kikatiba Mahakama Kuu ya Tanzania lilofunguliwa na Watanzania sita wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi dhidi ya Serikali, kupinga sheria inayozuia uraia pacha.

Kesi hiyo ya Kikatiba namba 18 ya mwaka 2022 imefunguliwa Mahakama Kuu Masjala Kuu na Shaban Fundi, Patrick Nyelesa Nhigula, Restuta Kalemera, Nkole Muya, Emmanuel Emmanuel na Bashir Kassam dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live