Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe alia na Sabaya

Mbowe IWD Mbowe alia na Sabaya

Mon, 21 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe amekumbusha machungu ya utawala wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya huku akidai kuwa, baadhi ya ofisi za umma nchini zinatumika kunyanyasa wananchi.

Mbowe, aliyekuwa mbunge wa jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, aliyasema hayo juzi alipokanyaga ardhi ya kijijini kwake tangu alipoondoka Julai 2021 na kukamatwa na Polisi na kuhusishwa na kesi ya ugaidi na uhujumu uchumi, kabla ya kesi hiyo kufutwa Machi 4, 2022.

Akizungumza katika mkutano wa mapokezi, Mbowe alimshukia Ole Sabaya ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa ya unyang’anyi na kutumia vibaya ofisi ya umma.

“Mungu hutenda kazi yake kwa miujiza. Ametenda miujiza kupitia kesi ya Mbowe. Sina hakika kama niwahukumu ama niwashukuru walionipeleka gerezani. Kwa sababu kuna wakati nilijiuliza, hao wenzetu wanafikiri kwa kutumia nini.

“Hawaioni dunia inaelekea wapi au wamekuwa vipofu. Maandiko matakatifu yanatufundisha kwamba Mungu aliamua kumtia Farao upofu na kiburi ili nini? Mungu aliamua kuwatia upofu na roho ya kiburi ili jambo fulani likadhihirike,” alisema Mbowe.

Alisema hata kukamatwa kwake kilikuwa ni kilele cha uonevu ambao ulikuwa umetamalaki nchi nzima, huku akiitaja Wilaya ya Hai kuwa kielelezo cha kunyanyaswa na kuumizwa watu.

Sabaya aliwahi kumtangazia Mbowe kuwa mwisho wa kutawala jimbo hilo umefika.

Akizungumza Septemba 8, 2019, katika kampeni ya Manyara ya kijani iliyozinduliwa mjini Babati na Mwenyekiti wa UVCCM Kheri James, ambaye (sasa DC Ubungo), Sabaya alisema;

“Mimi nimetumwa na Rais Magufuli kuwa DC wa Hai, lakini nimeteuliwa na Mwenyekiti wa CCM, mambo ya kuwa ‘neutral’ (kutokuwa na upande) mnayajua ninyi wenyewe. Mimi ni DC na nitawatangazia leo kwamba, kule Hai ufalme umeshafitinika,” alisema Sabaya.

Kutokana na madai ya kunyanyasa wananchi, Mbowe alidai jana kuwa, aliwashauri viongozi, akiwamo hayati Rais John Magufuli kuhusu uteuzi wa Sabaya lakini hakusikilizwa.

“Mimi nilipiga kelele muda mrefu. Niliiambia dunia, nikimwambia Rais Magufuli. Nikimwambia Waziri Mkuu, nimewaambia maspika, nimewaambia mawaziri, IGP kwamba jimbo la Hai mmetupelekea mhuni kuwa kiongozi wa watu,” alidai Mbowe.

Aliendelea; “Hao wote wananiambia Mheshimiwa Mbowe tutashughulikia, wakinigeuka wanacheka, tumempatia. Nimepatiwa Sabaya? Ofisi ya umma, ofisi yenu ya Serikali inatumika kutesa wananchi. Watu wamekatwa masikio?

“Hayo makosa anayoshitakiwa Sabaya ni asilimia moja ya uhalifu alioufanya katika nchi hii,” alidai Mbowe.

Hivi karibuni Mbunge wa jimbo hilo, Saashisha Mafuwe akikaririwa akimkaribisha kiongozi jimboni humo na kwamba hana kinyongo naye.

Lakini Mbowe akizimzungumzia mbunge huyo, alisema; “Hata huyo Mbunge nilimwambia huo ni ubunge wa damu hauna baraka.”

Huku akibainisha mambo aliyozungumza na Rais Samia baada ya kutoka gerezani, Mbowe alisema: “Mama Samia nimemwambia, Rais ukitaka tuelewane tuzungumze neno haki, kakubali namshukuru kwa hilo.”

Akizungumzia mapokezi yake wilayani humo kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mbowe alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kulinda amani.

“Hii ndio Tanzania tunayoitaka,” alisema. Awali mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila alimweleza Mbowe kuwa alipoachiwa tu alijitokeza mtu ambaye hakumtaja, na kueleza kuwa amemuomba msamaha lakini wakati akitamka hayo, Mbowe hakuwa na simu.

Mapokezi yalivyokuwa

Kabla ya kumpokea, shamrashamra zilianza mapema asubuhi ambapo magari ya wanachama na wafuasi wake kutoka mikoa mbalimbali ikiwamo ya Manyara, Arusha, Singida na Tanga yalionekana yakielekea uwanja wa ndege wa KIA.

Miongoni wa wanachama wa Chadema waliosafiri, mkazi wa Singida Mashariki ambaye alisafiri hadi Hai kushiriki mapokezi hayo, Evarist Bakari alienda mbali na kueleza wamebeba mbuzi wawili na watamkabidhi Mbowe ili atengeneze supu ili kutengeneza afya aliyoipoteza akiwa gerezani.

Mbowe alitua uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) 4:30 asubuhi kisha msafara wake ukaanza safari kuelekea mji wa Bomang’ombe, lakini ulipofika Njiapanda ya KIA, Mbowe alilazimika kuwasalimu wafuasi wake na wananchi.

Tukio lililoshangiliwa na wanachama na wafuasi wa Chadema na baadhi ya wananchi walioshiriki mapokezi hayo, ni la kutambulishwa kwa walinzi watatu wa Mbowe, ambao ni makomandoo wa zamani wa Jeshi la Wananchi.

Walinzi hao, Mohamed Ling’wenya, Halfan Bwire na Adam Kusekwa ambao walishitakiwa pamoja na Mbowe kabla mashitaka dhidi yao kuondolewa, hawakutambulishwa tu, bali walipewa zawadi ya mashuka ya Kimasai. Baadhi ya wananchi wa Hai ambao walishiriki katika mapokezi hayo walisema angalau sasa watalala usingizi kwa kuwa kwa siku zote 227 ambazo Mbowe alikuwa gerezani hawakupata usingizi mzuri, lakini sasa watalala vizuri.

Mwanasiasa huyo ambaye ni maarufu jimbo la Hai kwa jina la Kaka, alipokelewa na mabango yenye ujumbe “Pole Kaka. Nguvu ya mfalme ni Watu”, amekuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi vitatu 2000-2005, 2010-2015 na 2015-2020.

Usiku wa kuamkia Julai 8, 2021, familia ya Mbowe ilimpoteza kaka yao aitwaye Charles Mbowe, ambaye alizikwa Julai 12 na baadaye Mbowe akaondoka kijijini hapo hadi alipokamatwa na Polisi jijini Mwanza Julai 21 na kushitakiwa kwa ugaidi.

Katika eneo hilo, baadhi ya wafuasi walikuwa wamebeba mabango yenye picha ya Mbowe na mengine yakiwa na maneno kwa lugha ya Kichaga “Kwasha Kaka. Funya ya Mangi n Vandu” ikiwa na maana “Pole kaka. Nguvu ya mfalme ni watu.”

Msafara wake kutoka Njiapanda ya KIA hadi ofisi za Chadema zilizopo mji wa Bomang’ombe ulitanguliwa na pikipiki za vijana wa Bodaboda na baadaye magari, huku pembezoni ya barabara ya KIA-Hai, baadhi ya wananchi wakipunga mikono.

Akiwa ofisi za Chadema wilaya ya Hai, wazee wa chama hicho wakiongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa chama hicho Jimbo la Hai, wakiongozwa na Joen Nkya, walimkabidhi ngao na mkuki kama ishara ya ulinzi na amani.

Walichokisema wananchi wa Hai

Irene Lema ambaye ni mkazi wa Machame, alisema walipokea kwa mshituko taarifa za Mbowe kuhusishwa na ugaidi na siku zote walijua ni tuhuma za kutengenezwa, lakini wanamshukuru Mungu yuko huru na amerejea nyumbani.

“Sisi ambao ni wenyeji wa Hai tulijua ni tuhuma za kubambikiwa na tulimuomba Mungu sana aionyeshe dunia juu ya uonevu huu. Mapokezi ya leo yanatoa ujumbe wa Freeman ni nani katika hili jimbo. Wenye akili wameelewa,” alisema.

Fredy Shayo alisema walishtushwa sana kusikia Mbowe amekamatwa na anatuhumiwa kuwa gaidi, na kwamba kwa sasa wana amani na furaha wakiamini kiongozi wao ataendeleza mapambano ya kudai Katiba mpya, kwani sio ugaidi.

“Tulishangaa mtu anayedai Katiba mpya akawekwa ndani kwa ugaidi, leo yupo huru na amekuja, tunajisikia vizuri na tunamshukuru Mungu amesikia sala zetu na kuwezesha Kaka (Mbowe) kuwa huru na tunataka aendeleze moto huo huo.”

Imeandikwa na Daniel Mjema, Janet Joseph na Florah Temba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live