Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe ajitetea, afufua makaburi

83047 Mbowe+pic Mbowe ajitetea, afufua makaburi

Fri, 8 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (58) ameanza kujitetea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuishutumu CCM kuwa imeshindwa kutekeleza ndoto ya Watanzania ya kuwajengea maisha bora na ustawi.

Mbowe aliyaeleza hayo jana mbele ya hakimu Thomas Simba na jopo la mawakili wa Serikali likiongozwa na Faraja Nchimbi, huku yeye akiongozwa na wakili Peter Kibatala.

“Chadema tunaamini CCM imeshindwa kutekeleza ndoto ya Watanzania ya kujenga maisha bora na ustawi wao, kwa sababu kumekuwapo na matukio mbalimbali kwenye nyanja za ulinzi, usalama na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.” alieleza.

Alitoa mifano ya matukio mbalimbali yaliyowahi kuwafika likiwamo la yeye mwenyewe kushambuliwa kwa bomu akiwa mkutanoni eneo la Soweto jijini Arusha na kusababisha vifo vya watoto na wanawake.

Mbowe alidai katika tukio hilo hakuna mtu yeyote aliyewahi kufikishwa mahakamani. Pia, alieleza kuwa maombi yao ya kutaka uchunguzi wa tukio hilo ufanywe na watu kutoka nje ya nchi yalikataliwa.

Alidai kuwa kuna viongozi wao mbalimbali wameuawa kwa utata kwa nyakati tofauti, wakiwamo wanahabari na wanaharakati.

Mbowe ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo inayowakabili viongozi tisa wa chama hicho, alidai mwandishi wa habari Daud Mwangosi aliuawa na polisi eneo la Nyororo mkoani Iringa.

Hata hivyo, aliiambia Mahakama kuwa awali kamanda wa polisi mkoa wa Iringa alielekeza tuhuma kwa Chadema kuhusiana na mauaji hayo, mahakama ikathibitika polisi ndiyo walioua.

Pia, alidai kifo cha Alphonce Mawazo aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Busanda mkoani Geita 2015, aliuawa kwa kupigwa mapanga mita chache kutoka kituo cha polisi saa 5:00 asubuhi na alifariki saa 7:00 mchana bila msaada wowote.

Alieleza kuwa kulikuwapo na mazingira ya kutatanisha kutokana na Polisi kupiga marufuku shughuli za kumuaga hadi walipokwenda Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na kupata kibali.

Kuhusu msaidizi wake, Ben Sanane, Mbowe alidai alitekwa takriban miaka miwili iliyopita na waliiomba Serikali kuleta wachunguzi wa kimataifa lakini ilikataa.

Mfano mwingine, Mbowe alidai Daniel John aliyekuwa katibu kata ya Kinondoni alikamatwa na gari ya walinzi wa CCM akiwa na mwenzake wakapigwa na kuteswa.

Kuhusu tukio la kushambuliwa kwa aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbowe alieleza kuwa lilitokea saa 7:00 mchana Septemba 7, 2017 Dodoma na hadi sasa hakuna uchunguzi uliofanyika, hakuna taarifa ya kufikishwa mahakamani kwa mtu yeyote akihusishwa.

Baada ya Mbowe kueleza hayo, Kibatala akimuongoza alimtaka aiambie Mahakama njia wanayoitumia kuiondoa madarakani Serikali ya CCM.

Hata hivyo, kabla Mbowe hajajibu, wakili wa Serikali Joseph Pande alilipinga swali hilo kwa madai halihusiani na mashtaka yanayowakabili.

Mbowe aliendelea kueleza kuwa katika mchakato wa uchaguzi mawakala wakishateuliwa na chama husika kinawatambulisha kwa msimamizi wa uchaguzi ambaye anawaapisha siku saba kabla ya uchaguzi na kuwapatia utambulisho.

“Kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi mawakala wa vyama vya siasa wanastahili kupewa utambulisho lakini uchaguzi wa marudio wa Kinondoni hadi siku moja kabla ya uchaguzi kati ya mawakala wetu 611, ni 60 waliopewa tena siyo kwa wakati,” alidai.

Aliongeza kuwa kufuatia hali hiyo, Februari 16, 2018 ilikuwa siku ya mwisho ya kufunga kampeni mawakala hao walikuwa wakisubiri utambulisho huo katika ngome yao ya uchaguzi.

Alidai walikuwa umbali usiopungua mita 300 kutoka ofisi ya msimamizi wa uchaguzi na wengine walikwenda kusubiria ofisi ya msimamizi wa uchaguzi.

Alidai jambo hilo lilikuwa la msingi kwa sababu kwa kukosa utambulisho huo chama kingekosa mawakala, ambao wanawajibu wa kusimamia maslahi yake.

Alidai siku hiyo walikuwa wanafunga kampeni na kulikuwa na hamasa kubwa na mwingiliano wa watu.

Chanzo: mwananchi.co.tz