Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe aanika mikakati ya 2023

Mbowe Pic 1140x640.jpeg Mbowe aanika mikakati ya 2023

Sat, 17 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amewataka wenye ndoto ya kuwa wabunge au mameya wajipange kuanzia Januari mosi mwakani kwa kuwa, hakuna njia ya mkato kufikia mafanikio.

Mbowe alisema hayo wakati akifunga semina ya waliokuwa wagombea ubunge wa chama hicho jijini Dar es Salaam juzi ikiwa ni siku chache baada ya kurejea kutoka ziarani Marekani.

“Kama hatutajipanga vizuri kuanzia sasa, hakuna njia ya mkato ya kuwa mameya, madiwani au wabunge. Matunda ya mwaka 2025, yatapatikana kuanzia mwaka 2023, kwa hiyo mwenye ndoto ya kuwa mbunge lazima ajipange mapema.

“Hakuna siri ya kujenga siasa bila kuwafikia wapigakura, hatuwezi kukesha katika mitandao ya kijamii na kudhani tutafanikiwa, tunadanganya. Lazima tushuke chini kwa wapigakura na tuna wajibu huo mkubwa... lazima tuufanye,” alisema Mbowe.

“Mwakani hatutashinda mitandaoni, tutahamia jimboni kuhamasisha Chadema Digital ili tusajili wanachama wengi, tutashirikishana, tutalazimishana na tunakwenda kufanya kazi.”

“Mimi mwenyewe nitafanya operesheni ya jimbo kwa jimbo, kata kwa kata. Yaani kuanzia Januari mwakani ni operesheni kama zile za M4C, tunakwenda kukipanga chama na sitafanya mimi, tutafanya wote na makao makuu yetu, tutahamia majimboni,”alisema Mbowe.

Alisema wakati wa operesheni ya M4C ilikuwa mtu anatoka Arusha anakwenda Mwanza, anatoka Katavi anakwenda Kigoma, “lakini kwa miaka saba hii tulizuiwa, sasa kuanzia Januari tunaanza tena.”

“Kwa nchi yetu, ajenda zipo kibao za kwenda nazo kwa wananchi. Uzuri ni kwamba Chadema hatujawahi kukosa ajenda. Ukigusa umeme, maji, elimu zote hizi ni ajenda,” alisema Mbowe.

Katika semina hiyo, kulifanyika uchaguzi wa spika na naibu wa wabunge wa wananchi huku Susan Lyimo akiibuka mshindi wa uspika baada kupata kura 50 dhidi ya mpinzani wake Celestine Simba aliyepata kura 35.

Lumola Steven alipata kura 69 za ushindi wa unaibu na kumshinda Shija Shibesh aliyepata kura 16. Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Kigaila Benson akimkaribisha Mbowe akisema kikao hicho kilifanyika kwa siku mbili (juzi na jana) na kilikuwa na malengo makubwa mawili kwanza kupeana mafunzo ya namna gani wanafanya kama wabunge kuelekea mwaka 2024/25.

Alisema mada mbalimbali ziliwasilishwa na kuchangiwa na washiriki wa semina hiyo, “watu hawa tumeongea nao kwa kina na tumekubaliana wanakwenda kufanya kazi kwenye majimbo yao kwa nguvu kubwa, ili kila mmoja ajihakikishie atakuwa mgombea katika uchaguzi ujao.”

Baada ya kutangazwa mshindi, Lyimo aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu, aliwashukuru kwa kumchagua na kuwahakikishia kujenga bunge lenye umoja litakalokuwa linapaza sauti ya wananchi. Pia, aliahidi kukutana na kamati ya uongozi kuangalia namna ya kuwa na bunge lenye muundo utakaofanya wabunge wote washiriki kikamilifu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live