MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema agizo la kuwataka wabunge wa chama hicho kujiweka karantini kwa siku 14, halikuwa uamuzi wake binafsi bali wa chama.
Mbowe alitoa kauli hiyo jana, akieleza kuwa wabunge waliokaidi agizo hilo, watavuna walichokipanda.
Alisema chama hakiwezi kumzuia yeyote kukihama na kina matarajio ya kupata wabunge wengi wapya katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
“Lazima utambue kwamba kila kwenye mzunguko wa uchaguzi, uchaguzi wa ndani ya chama au wa kiserikali kwa maana ya uchaguzi mkuu, wanatoka watu na wanaingia wengine wapya. Kila mtu atavuna alichokipanda," alionya.
Kauli hii ya Mbowe imekuja siku moja baada ya Mbunge wa Momba na Katibu wa Wabunge wa Chadema, David Silinde, kutangaza kujiuzulu nafasi yake hiyo na nyingine ndani ya chama baada ya wabunge wa chama hicho kumtaka ajiuzulu kwa kukaidi maelekezo ya kujiweka karantini.
Mbunge huyo alisema juzi kuwa alijivua nafasi ya ukatibu wa wabunge na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mbali na Silinde wabunge wengine wa Chadema waliokaidi agizo hilo ni pamoja na Mbunge wa Moshi Mjini, Jafari Michael, Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Msabaha, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali, na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, ambaye tayari ameshaweka wazi atakihama baada ya kufungwa kwa Bunge la 11.
Juzi, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alinukuliwa akisema uamuzi wa kuwazuia wabunge wa Chadema kuingia bungeni kushiriki shughuli za Bunge ni wa kibabe na uongozi wa Bunge haujapendezwa na hatua hiyo.
“Wabunge ni timu moja, huwezi kwenda katika timu unatoa tu wachezaji wako, 'tokeni', hata hujajadiliana na wenzako, hamjazungumza, na hii ndiyo ‘dictatorship’ (ubabe) inayozungumzwa katika chama cha Chadema," Spika Ndugai alilalamika.
Hata hivyo, Spika Ndugai alisema maelekezo hayo kwa wabunge wa Chadema hayana athari yoyote kwa Bunge kuendelea kwa kuwa idadi ya wabunge wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni wengi kuliko wale wa upinzani na hivyo akidi kutimia kwa Bunge kuendelea.
KAULI YA SILINDE
Juzi, Silinde alisema agizo lililotolewa kwa wabunge wa Chadema kujiweka karantini kwa siku 14 lilitolewa kama tahadhari na siyo lazima.
Silinde alisema wakati huu taifa likichukua hatua za kukabiliana na maambukizo ya virusi vya corona, hakuona ulazima wowote wa kutoka bungeni na hakuna manufaa yoyote ambayo yangetokana na uamuzi huo.
Mbunge huyo alisema hatua ya kutohudhuria vikao halali vya Bunge vitawakosesha wananchi haki yao ya kuwakilishwa katika mojawapo ya chombo hicho kikuu cha uamuzi na hivyo kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Niliamua kuendelea kuhudhuria vikao vya Bunge kwa kuwa agizo la mwenyekiti halikuwa la lazima, bali mimi nalichukulia kama ilikuwa tahadhari kwa kuwa historia inaonyesha maambukizo hayo yamepatikana maeneo tofauti na bungeni,” alisema.
Silinde alisema kabla ya Mbowe kutoa agizo hilo wiki iliyopita, hakukuwa na mawasiliano wala makubaliano ya pamoja miongoni mwa wabunge wa chama hicho kuhusu uamuzi huo na aliamini ulipaswa kupata kwanza uungwaji mkono na wengi.
Katika hatua nyingine alisema kwa sasa hakuna mgawanyiko katika chama hicho ingawa baadhi ya wakosoaji ndani na nje ya chama hicho wanadhani kutokubaliana na mawazo ya mwenyekiti ni usaliti na utovu wa nidhamu badala ya kuonekana kama haki ya uhuru wa kutoa maoni.
“Kuna baadhi ya wakosoaji wa hatua hii ambayo baadhi yetu tumechukua ya kuendelea kuhudhuria vikao vya Bunge kutoka ndani na nje ya chama wakidai sisi ni wasaliti au watovu wa nidhamu, lakini ni utaratibu wa kawaida wa uhuru wa kutoa maoni bila kuathiri kanuni za chama,” alisema.
Alisema kwa sasa ataendelea kuhudumia wananchi wake akiwa mwakilishi mbunge kupitia Chadema na iwapo kutakuwa na ulazima wa kuhamia kwingineko, atawasiliana na wapigakura wake ambao wataamua hatima yake kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
“Mimi sijanunuliwa kama baadhi ya watu wanavyodai na kwa sasa bado mbunge kupitia Chadema, iwapo kutakuwa na ulazima wa kuhama, nitafanya uamuzi kutegemea mawazo ya wapigakura wa Momba hususan wakati wa uchaguzi mkuu ujao na siyo vinginevyo," alisema.