Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na makamu wake mpya, Tundu Lissu baada ya kuchaguliwa jana, wamesema kazi iliyo mbele yao ni kuhakikisha chama hicho kinashinda uchaguzi mkuu wa 2020.
Viongozi hao walisema wana kibarua kizito cha kukiandaa chama hicho ili kiweze kukabili changamoto za uchaguzi wa rais na wabunge utakaofanyika mwakani.
Mbowe na Lissu wamedai baada ya kumalizika uchaguzi wa ndani wa chama chao sasa nguvu yao wanapaswa kuelekeza katika kuhakikisha wanakamata dola.
Katika uchaguzi wa jana, Mbowe alichaguliwa kuwa mwenyekiti wakati Lissu akiibuka kidedea kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti kwa upande wa Tanzania Bara na Said Mohamed Issa akitetea kiti chake cha umakamu kwa upande wa Zanzibar.
Mchakato wa uchaguzi wa chama hicho ulikuwa unatazamiwa kumalizika jana usiku kwa Baraza Kuu la chama hicho kuteua Katibu Mkuu na manaibu wake wawili.
Hadi jana kulikuwa na hatihati ya Dk Vincent Mashinji kuendelea kuwa Katibu Mkuu huku jina la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika likichomoza.
Huku Benson Kigaila na John Mrema wakitajwa mmoja wao anaweza kuwa Naibu Katibu Mkuu upande wa Tanzania Bara, ambayo ni nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Mnyika.
Kwa Naibu Katibu Mkuu upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu alikuwa anapewa nafasi kubwa kuendelea katika nafasi hiyo.
Pia makada 17 wa Chadema walikuwa wanagombea nafasi nane za ujumbe wa Kamati Kuu.
Walitakiwa kuchaguliwa wajumbe sita wa upande wa Tanzania Bara na wawili kwa upande wa Zanzibar.
Hadi gazeti hili linaenda mitamboni jana saa tano usiku, mchakato wa kuwapata viongozi hao ulikuwa ukiendelea katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Mikakati ya 2020
Mbowe aliyainisha mambo matatu atakayoyawekea mkazo katika kuhakikisha chama hicho kinazidi kuwa imara hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa hotuba fupi ya kuwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho kwa kumchagua.
Alisema mikakati hiyo ni pamoja na kusimamia nidhamu ndani ya chama hicho, kusukuma mambo kwa lengo la kuhimiza utendaji wa shughuli za chama hicho sambamba na kuhakikisha ngazi zote za chama hizo zinafanya kazi kwa ufanisi.
“Kuanzia sasa tunapotoka katika ukumbi huu mashina ya chama, mabaraza, vijana, wazee, kina mama wote mkafanye kazi.
“Tutasukumana sana kuliko ilivyokuwa kawaida, tutajenga nidhamu kwa kasi kali. Tutasukumana kwa makundi lakini haya yote tutafanya kwa nia njema, kila mmoja mwenye dhamana atambue, ili malengo yetu ya pamoja yawezeshe kesho yetu iwe bora kuliko jana,” alisema Mbowe kwenye hotuba hiyo aliyoitoa saa 11 alfajiri.
Lissu
Lissu, ambaye alichaguliwa licha ya kuwa nje ya nchi alieleza jukumu kubwa ni kukiandaa chama kukabili majukumu makubwa na magumu ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Alisema uchaguzi wa ndani umeisha na viongozi wamepatikana sasa kazi yao ni kuandaa mikakati ya kufanya chama hicho kuwa vizuri.
“Sitakaa nje milele. Pia kuna njia nyingi na rahisi za mawasiliano. Wanachama wamethibitisha kwenye uchaguzi huu, inawezekana kuwasiliana na kufanya kazi za chama hata nikiwa nje,” alisema Lissu wakati akizungumzia kitendo cha kuchaguliwa pamoja na kuwa nchini Ubelgiji ambako amekuwa anaishi tangu alipokumbwa na shambulio la risasi.