Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameondoka nchini kuelekea Italia kwa ziara ya kikazi ya siku nne.
Katika safari hiyo, Mbowe ameambatana na viongozi wengine wawili wa chama hicho, Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu na Katibu Mkuu, John Mnyika.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu Juni 5, 2023 katika taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema.
Kwa mujibu wa Mrema kupitia taarifa hiyo Lissu na Mnyika watatangulia kurejea nchini Juni 7, mwaka huu wakati Mbowe akiendelea na ziara kwingineko.
Imeelezwa kuwa Mwenyekiti huyo baada ya kuhitimisha ziara ya Italia, atakwenda Ujerumani kwa ziara ya siku mbili.
Atakapokuwa Ujerumani kulingana na taarifa hiyo, atakutana na viongozi mbalimbali wa kisiasa, Serikali na Mashirika ya Kimataifa na kwamba atarejea nchini Juni 10 mwaka huu.