Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema anatamani kwenda Ikulu kukutana na Rais John Magufuli akiwa na timu ya viongozi wenzake waandamizi na si yeye peke yake.
Mbowe amesema hayo ikiwa ni siku mbili kupita tangu Rais Magufuli akutane kwa nyakati tofauti na viongozi watatu wa vyama vya upinzani Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya nao mazungumzo ya faragha.
Hata hivyo, Mbowe alisema hajawahi kupokea mwaliko wa kwenda Ikulu. “Mimi binafsi sijawahi kuitwa,” alisema Mbowe alipozungumza na Mwananchi jana, huku akisema hawezi kuwazungumzia viongozi waliokwenda kwa sababu hafahamu walichokizungumza na rais.
Viongozi hao ni Mshauri mkuu wa ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba na wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu Jumanne ilieleza kuwa mazungumzo hayo yalijikita katika masuala ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu na kuhimiza haja ya kudumisha amani, usalama na upendo.
Baada ya mazungumzo kulikuwa na taarifa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Mbowe alialikwa lakini akagoma kwenda kutokana na ushauri aliopewa na viongozi wenzake.
Habari zinazohusiana na hii
- VIDEO: Walichozungumza Maalim Seif, Mbatia na Lipumba baada ya kukutana na Magufuli
- VIDEO: Maalim Seif asema bila ushirikiano wapinzani ngumu kushinda uchaguzi mkuu 2020
- VIDEO: Maalim Seif aweka wazi alichozungumza na Rais Magufuli
- Maalim Seif: Magufuli akutane na wapinzani wote kujadili uchaguzi huru na haki - VIDEO
“Tungetamani kukutana na Rais, lakini tuitwe Chadema kama taasisi tutakwenda kukutana na Rais na yeye awe na timu yake tujadili na tubadilishane mawazo, siyo niitwe Mbowe kama Mbowe nikakutane na Rais. Natamani sana niende na timu ya viongozi wangu,” alisema mbunge huyo wa Hai na kusisitiza:
“Kwa nini niende peke yangu, tunapozungumza mambo makubwa yenye mustakabali wa nchi hayahitaji kuwa ya mtu mmojammoja, tukae kama timu tuzungumze kwa pamoja,” alisema.
Mbowe alisema tangu alipomwandikia barua Rais Magufuli Januari 29 kuhusu mambo yanayopaswa kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu haijawahi kujibiwa.
“(Barua) Haijawahi kujibiwa wala kuonyesha tu kuwa imemfikia, kwa hiyo ni imani yangu kama tutaitwa tutakwenda na sitamani kwenda peke yangu, mambo ya nchi yanajadiliwa kwa upana na Rais akiwa na timu yake,” alisema.
Februari 3, Mbowe akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam alisema amemwandikia barua Rais Magufuli iliyokuwa na mambo matatu ikiwamo kumwomba aunde tume ya maridhiano kujadili hali ya siasa nchini.
Mambo mengine ni kutaka uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24 mwaka jana kufutwa na kurudiwa pamoja na marekebisho ya Katiba kufanyika ili kuruhusu kuwa na tume huru ya uchaguzi.
Uchaguzi wa serikali za mitaa ulifanyika huku ukishuhudia vyama vya Chadema, ACT- Wazalendo, NCCR-Mageuzi, Chadema, Chaumma na UPDP vikiususia kwa kile walichodai kufanyiwa figusi kwa wagombea wao kuenguliwa kabla na baada ya kuchukua fomu.
Maombi ya Mbowe kutaka kukutana na Rais akiwa na timu ya viongozi wenzake na maudhui ya barua yake kwa Rais yanafanana na kile alichokisema katika sherehe za maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, mwaka jana jijini Mwanza alipoomba kufanyika kwa maridhiano kuelekea uchaguzi mkuu ili uwe huru na haki.
Msingi wa kuandika barua ya kuhitaji maridhiano ni pamoja na masuala yanayoendelea nchini kuhusu suala zima la usalama na kesi za kisiasa zinazowakabili wanasiasa na kuwapo katazo la kufanya siasa.
Anachokisema Mbowe kinashabihiana na ushauri uliotolewa na Maalim Seif kwa Rais Magufuli, akimtaka akutane na viongozi wote wa vyama vya upinzani kwa pamoja kujadili masuala ya uchaguzi mkuu, likiwamo suala la kuwa na tume huru ya uchaguzi.