Kufuatia mfululizo wa matukio ya utekaji na mauaji ya wananchi na viongozi wa chama chake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema hawatarudi nyuma katika kutetea haki katika taifa hili.
Mbowe amebainisha hayo leo Alhamisi, Septemba 19, 2024 wakati wa mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) wenye lengo la kutathmini hali ya demokrasia nchini ikiwa ni sehemu ya tafakuri ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia inayoadhimishwa kila Septemba 15 kila mwaka.
Amesema mwezi huu, chama hicho kimekuwa kwenye maombolezo kufuatia matukio ya utekaji na mauaji ya viongozi wake na vyombo vya dola kutokuwa na majibu kuhusu wahusika wa matukio hayo ili wafikishwe kwenye mkondo wa sheria.
Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa TCD, viongozi wa chama chake wamekuwa wakipotea katika mazingira ya kutatanisha huku akitolea mfano Katibu wa Chadema, Jimbo la Sumbawanga, Dioniz Kipanya ambaye amepotea wiki sita zilizopita.
Mbali na Kipanya, Mbowe amesema Katibu wa Vijana wa chama hicho Bavicha, Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na wenzake wawili, Jacob Mlay na Frank Mbise, haijulikani walipo.
Mwenyekiti huyo wa TCD amesema, wakiwa hawajapata majibu ya viongozi hao walipo, kiongozi aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya chama hicho, Ali Kibao akatekwa na watu wenye silaha, Septemba 6, 2024 kisha mwili wake ukaonekana umetumwa, Ununio.
Kibao alitekwa na watu, jioni ya siku hiyo, eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam, akiwa ndani ya basi la Tashrif akielekea nyumbani kwake, jijini Tanga. Wakati Chadema na wadau wengine wakihoji alipo, mwili wake ukaonekana Ununio.
Mbowe amesema katikati ya hayo yakiwa yanaendelea na kutokupata majibu, jana Jumatano, aliyekuwa meya wa Ubungo, Boniface Jacob amekamatwana Polisi na anaendelea kushikiliwa na Polisi katika kituo cha Osterbay.
"Hatutarudi nyuma katika kutetea haki katika taifa hili. Kama tunataka kwenda mbele, lazima tuwe jasiri kusimama na kusema ukweli," amesema Mbowe wakati wa mkutano huo.
Ameongeza kuna haja ya kupata vyombo huru vya kuchunguza matukio hayo kwani kila mmoja ana thamani yake kipekee, hivyo kupotezwa kwa watu ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Mwanasiasa huyo amesema Katiba inatambua haki ya msingi ya kuishi bila kujali rangi yake, imani yake au mahali anakotokea, lakini katiba haifuatwi katika kusimamia maisha ya watu.
Mwenyekiti huyo amesema chama hicho kinatamani wakati wote nchi iongozwe na Katiba iliyo bora ili kutengeneza ustawi ulio bora kwa wananchi wote na si utash wa kiongozi mmoja.
“Tunaamini Katiba iliyo bora itazaa sheria bora na vyote kwa pamoja vitatengeneza ustawi uliobora kwa raia wote. Nayazungumza haya nikiamini kwa muda mrefu katika nchi yetu kumekuwa na utamaduni wa walioko katika madaraka kuamini utashi wa kiongozi mkuu ndiyo unapaswa kuwa Dira ya Taifa.
“Dira ya Taifa letu wakati wote ili iwe ya haki kwa makundi na watu wote haipaswi kuwa utashi wa kiongozi mkuu, inapaswa kuwa imechimbiwa kwenye katiba ya nchi,” amesema Mbowe.