Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe: CHADEMA tukikanyaga Ikulu tunaanza na uraia pacha

Mbowe Lissu Dar Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

Fri, 3 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kikiingia madarakani, kitaweka utaratibu wa uraia pacha kwa kila Mtanzania atakayehitaji.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema hayo wakati akizungumza katika mikutano tofauti akiwa mkoani Njombe juzi ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya hadhara ya chama hicho katika Kanda ya Nyasa.

Alisema nchi nyingi duniani zimeweka utaratibu wa wananchi wake kuwa na uraia pacha na kutokana na utaratibu huo umesaidia kuziongezea pato kwenye nchi zao.

“Na huo ni mtaji mkubwa wa kuongeza pato la taifa kwa sababu vijana wengi wanapata ajira, wakikosa katika nchi moja wanakwenda kupata katika nchi nyingine.

“Siku mkitupa serikali sisi CHADEMA, Watanzania wote wanaotaka uraia wa nchi yoyote, watapata. Wewe ukisoma hapa huna ajira, kama unaweza ukaenda Dubai ukapata kazi nenda na ukipata uraia sawa. Tutahakikisha vijana wote wanaokosa ajira kwenye nchi hii wanapata uwezo wa kwenda nchi nyingine kutafuta ajira.”

Mbowe alisema idadi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi bado ni ndogo.

"Katika kila Mtanzania mmoja aliyeko nje, raia wa nchi nyingine ya Afrika Mashariki wako 20, serikali zao zinawapa uhuru. Msimamo wa CHADEMA ni kufika hapo, lakini tunasema ili kufika hapo ni lazima tulete mabadiliko makubwa ya Katiba.

“Tunataka kuhakikisha kwamba sisi kama chama kikubwa kazi yetu ya kwanza ni kupata Katiba mpya, ili viongozi wote wakatokane na chaguzi zilizo huru na haki.”

Mbowe alisema wamehitimisha ziara kwa mkutano wa hadhara mjini Iringa mjini na baada ya hapo wataelekea mikoa ya Kaskazini kuendelea na mikutano hiyo.

"Tumetokea Mbarali ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini au Kanda ya Nyasa. Kesho tutamalizia mkutano mkubwa katika viwanja vya Iringa mjini na asubuhi tutaanza na Mafinga.”

Mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekiel Wenje, alisema katika maeneo yote waliyopita katika ziara hizo, kilio kikubwa cha wananchi ni ukosefu wa maji.

"Kila kona ya Tanzania tulipokwenda, watu bado wanalia maji. Miaka 60 ya uhuru watu bado wanakosa maji na wanaona kawaida, kwenye uchaguzi unaokuja, wajibisheni hii serikali iliyopo madarakani kwa kuiondoa.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live