Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imepanga Desemba 14, 2023 kutoa hukumu katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na wabunge 19 wa Viti Maalumu akiwamo Halima Mdee, ambao walifukuzwa Uanachama katika Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema).
Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne Oktoba 24, 2023 na Jaji anayesikiliza shauri hilo, Cyprian Mkeha wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya hukumu.
Kupangwa kwa tarehe hiyo ya Hukumu kunatokana na wabunge hao 19 kufunga usikilizwaji wa kesi yao dhidi ya chama hicho, Septemba 7, 2023 baada ya kumaliza kuwahoji mjumbe wa sita wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema.
Baada ya wabunge hao kumaliza kuwahoji wajumbe hao siku hiyo, Jaji Mkeha alielekeza pande zote wapewe nakala za mwenendo wa kesi hiyo Septemba 21, 2023 na pande zote wawasilishe mahakamani majumuisho ya hoja zao Oktoba 19,2023.
Wabunge hao akiwamo Halima Mdee ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na wenzake 18 walifungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu, wakipinga kufukuzwa uanachama, kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review).
Jopo la mawakili wa kina Mdee, Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashu liliwaita mahakamani wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema ili kuwahoji pamoja na mambo mengine kuhusiana na uhalali wa utaratibu uliotumika kuwavua uanachama kina Mdee.
Hata hivyo, leo Oktoba 24, 2023 Jaji Mkeha amesema kesi hiyo imeitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama pande zote zimekamilisha kuwasilisha hoja na kisha kupanga tarehe ya uamuzi.
"Kwa kuwa pande zote zimewasilisha hoja zao, Mahakama hii inapanga Desemba 14, 2023 kutoa hukumu dhidi ya shauri hili," amesema Jaji Mkeha.
Hata hivyo kesi hiyo ilisikilizwa chemba kwa maana ya mawakili wa pande zote ndio walioitwa mahakamani hapo na kupewa tarehe kwa ajili ya Hukumu hiyo, huku wananchama na wafusi wa pande zote wakibaki sehemu Maalumu iliyotengwa na Mahakama kwa ajili ya watu kukaa na kusubiri kuitwa kwa kesi zao.
Wabunge hao, Halima Mdee, na wenzake 18 wamefunga usikilizwaji wa kesi yao hiyo kupitia mwa mawakili wao, leo Alhamisi, Septemba 7, 2023, baada ya mawakili wao kumaliza kuwahoji wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema.
Mdee ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), na wenzake 18 wamefungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu, wakipinga kufukuzwa uanachama, kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review).
Katika kesi hiyo kina Mdee wanapinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema kutupilia mbali rufaa zao za kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kuwafukuza uanachama kwa tuhuma za kuapishwa kuwa wabunge bila ridhaa ya Chama.
Kamati Kuu iliwavua uanachama wa Chama hicho Novemba 27, 2020. Walikata rufaa Baraza Kuu kupinga uamuzi huo wa Kamati Kuu lakini Baraza Kuu katika uamuzi wake wa Mei 11, 2022, kulitupilia mbali rufaa yao hiyo.
Baada ya uamuzi huo wa Baraza Kuu kutupilia mbali rufaa yao, ndipo wakakimbilia mahakamani ambako kwanza waliomba na wakapata kibali kufungua shauri hili.
Wanapinga uamuzi wa Baraza Kuu pamoja na mambo mengine wakidai kuwa hawakupewa haki ya kusikilizwa, ambayo ni haki ya msingi.
Hivyo wanaiomba mahakama itengue mchakato na uamuzi huo, iamuru Chadema kutimiza wajibu wake kisheria, yaani kuwapa haki ya kuwasikiliza na itoe zuio kwa Spika na Nec kuchukulia hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapoamuriwa.
Mbali na Chadema kupitia Bodi yake ya wadhamini, wadaiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye pia anasimama niaba ya Bunge la Tanzania; na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Awali jopo la mawakili wa Chadema likiongozwa na Wakili Peter Kibatala liliwaita kwa amri ya Mahakama wabunge wanane kati ya 19 wafike kizimbani, akiwemo Mdee kwa ajili ya kuwahoji kuhusiana na malalamiko yao waliyoyaweka katika kiapo chao walichokiwasilisha Mahakamani ambao ni ushahidi wao.
Mbali na Mdee, wengine walioitwa walikuwa ni Nusrati Hanje, Ester Matiko, Ester Bulaya, Grace Tendega, Jesca Kishoa, Cecilia Pareso na Hawa Mwaifunga.
Hata hivyo mawakili wa Chadema waliamua kufunga mahojiano bila kuwahoji Mdee, Bulaya na Matiko, licha ya kuwaita.
Baada ya hapo ndipo jopo la mawakili wanne wa kina Mdee likiongozwa Ipilinga Panya walipowaita wajumbe hao wa Bodi ya Wadhamini Chadema waliosaini viapo kinzani walivyoviwasilisha mahakamani kupinga madai ya kina Mdee, ili kuwahoji kuhusiana na uhalali wa utaratibu uliotumika kuwabua uanachama
Waliohojiwa ni Dk. Azavery Lwaitama, Silivester Masinde, Ruth Mollel, Ahmed Rashid Hamis. Maulida Anna Komu na Francis Joseph Mushi, ambaye alikuwa wa mwisho, huku Mary Joachim ambaye alitakiwa kuhojiwa na mawakili wa kina Mdee kushindwa kufika mahakamani hapo kwa sababu ya ugonjwa.