Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbatia na wenzie wakimbilia Polisi

Mbatiaaa James Mbatia akizungumza

Mon, 20 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bodi ya Wadhamini ya Chama cha NCCR-Mageuzi, imefungua jalada la uchunguzi wa tuhuma za kuvunjwa kwa ofisi ya chama hicho, zinazodaiwa kufanywa na Kaimu Mwenyekiti wake, Haji Khamis na Katibu Mkuu, Martha Chiomba.

Jalada hilo limefunguliwa usiku tarehe 17 Juni 2022, saa chache baada ya Haji, Chiomba na baadhi ya wanachama wa NCCR-Mageuzi, kuvunja milango ya ofisi hiyo kisha kuingia ofisi na kufanya shughuli kadhaa za chama.

Akizungumza baada ya jalada hilo kufunguliwa, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya NCCR-Mageuzi, Samuel Ruhuza, amesema wamechukua hatua hiyo ili Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi kwa ajili ya kuchukua hatua kwa wahusika.

“Tumewapa kazi Polisi wafanye kazi yao kubaini hali halisi ilivyokuwa. Wao ni watalaamu watajua nini kimetokea, nani anawajibika na kwa nini wamefanya hivyo. Kama mfanyakazi yoyote ameacha kitu ofisini akija kikikosa atoe taarifa,” amesema Tuhuza.

Ruhuza amedai waliotekeleza kitendo hicho wana nia ovu kwa kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeita pande mbili zinazovutana katika mgogoro wa uongozi wa NCCR-Mageuzi, kwa ajili ya kupata usuluhishi.

“Ofisi ya Msajili ilituita viongozi tarehe 21 Juni 2022, twende ofisini tukazungumze ni kama zimebaki siku nne, nashindwa kuelewa kama una barua ya kuitwa ofisini kwa msajili leo vipi uvunje kufuli ufanye uvamizi wa ofisi? Una nini hasa unakitafuta ndani. Ni nia ovu,” amesema Ruhuza.

Mtandao huu umemtafuta Kamanda wa Polisi Ilala, ACP Debora Magiligimba, kuthibitisha kama jalada hilo limefunguliwa, ambaye amejibu “ siwezi kuongelea mafaili yanayofunguliwa kituoni, subiri kama limefunguliwa uchunguzi umekamilika mtapata maelezo.”

Tukio la kuvunja kwa milango ya ofisi hiyo limetokea wiki kadhaa baada ya Bodi ya Wadhamini ya NCCR-Mageuzi, kufunga ofisi za chama hicho na kuiweka chini ya uangalizi pamoja na mali zake, kwenye kampuni ya ulinzi ya Haraka Security Limited, hadi pale ufumbuzi wa mgogoro wa chama hicho utakapotafutiwa ufumbuzi.

Licha ya hatua hiyo, Khamis na Chiomba, jana walikwenda ofisini hapo wakiambatana na uongozi wa serikali ya mtaa, kisha kuvunja milango na kuingia ndani, ambapo walitekeleza shughuli kadhaa ikiwemo kutangaza wajumbe wapya wa sekretarieti.

Mgororo huo uliibuka baada ya Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi, kumsimamisha uongozi Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, pamoja na kuvunja sekretarieti yake.

Hata hivyo, Mbatia na wenzake wanadai uamuzui huo ni batili kwa kuwa kikao cha halmashauri hiyo kilichoketi mwishoni mwa Mei, 2022, kilikuwa batili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live