Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbatia ataka muda wa kuchukua fomu Serikali za mitaa kuongezwa

82702 Mbatia+pic Mbatia ataka muda wa kuchukua fomu Serikali za mitaa kuongezwa

Mon, 4 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amemtaka Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo kuongeza muda kuchukua fomu za uchaguzi wa Serikali za mitaa kutokana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza.

Wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa walianza kuchukua na kurejesha fomu kuwania uwenyekiti wa kijiji, mtaa, kitongoji na ujumbe wa kamati ya mtaa kuanzia Oktoba 29, 2019. Shughuli hiyo inayofanyika kwa siku saba itakamilika Novemba 4, 2019.

Akizungumza mjini Dodoma leo Jumamosi Novemba 2, 2019 Mbatia amesema baadhi ya maeneo ofisi zilifunguliwa siku mbili tu, baada ya hapo zilifungwa jambo lililowakosesha  nafasi wagombea wengine kuchukua fomu.

Amesema Serikali imetoa muda wa siku saba kwa ajili ya wagombea kuchukua na kurudisha fomu lakini baadhi ya vituo vinafungwa kabla ya muda.

“Ni tatizo kubwa kwa sababu haya yanayoendelea hakuna mwenye majibu, waziri hajui, katibu mkuu hajui, mkuu wa Mkoa hajui na katibu tawala wa Mkoa hajui.”

“Hakuna mwenye majibu ya moja kwa moja kuhusu hili, mbaya zaidi chama kilichopo madarakani kinalalamika na wapinzani wanalalamika, ni hali ya ajabu kabisa,” amesema Mbatia. Amedai baadhi ya maeneo ambayo vituo vimefungwa ni Wilaya ya Mbinga, Kilombero, Moshi, Dar es Salaam, Butiama, Mbeya, Karagwe, Liwale na Kwimba.

Amesema malalamiko ni mengi kila kona, na kumtaka Jafo kuongeza muda ili wenye nia ya kugombea kujitokeza kwa wingi.

Chanzo: mwananchi.co.tz