Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakili wataka wafuasi Chadema waachiwe huru

47889 Chadema+pic

Thu, 21 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi ya kufanya mikusanyiko isiyo halali wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwaachia huru watu 31 wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema.

Hatua hiyo imekuja baada ya wakili wa Serikali, Faraji Nguka kuieleza Mahakama hiyo kuwa shauri hilo lilikwenda kwa ajili ya maelezo ya awali ila wameshindwa kuandaa jalada kwa kuwa lipo polisi likiwa limeambatanishwa na hati ya kuwakamata baadhi ya washtakiwa.

"Tumeshatoa hati ya kukamatwa washtakiwa 15 hivyo tunaiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ili waweze kusomewa maelezo ya awali," ameeelza Nguka.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Alex Masaba ameeleza mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile  kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha sheria namba 27 ya mwaka 2018, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) inapotekeleza majukumu yake inatakiwa kutenda haki na isivunje taratibu za Mahakama.

Masaba amesema mwenendo wa mawakili wa Serikali tangu kesi hiyo imefunguliwa Februari 2018 mpaka sasa imefika miezi 13 ni dalili  kuwa haki ya washtakiwa imekiukwa.

Wakili huyo amedai taratibu za kimahakama zimekiukwa kwa mujibu wa kifungu cha 225(4) cha sheria ya mwenendo wa mashtaka ya jinai inayoeleza kuwa kesi inapofunguliwa inatakiwa ianze kusikilizwa kwa miezi sita lakini sasa imefika miezi 13.

"Tunaiomba Mahakama izingatie sheria ili iweze kusimamia haki za washtakiwa na taratibu za Mahakama na iwaachie uhuru kwa kuwa Jamhuri imekiuka taratibu za uendeshaji wa kesi," amedai Masaba.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Hakimu Rwizile amesema kesi itakapokwenda tena mahakamani hapo mawakili wa upande wa mashtaka wanatakiwa kuchagua kama waendelee na kesi bila washtakiwa hao kuwapo au ifutwe.

"Mimi nitatumia mamlaka yangu kuifutilia mbali hii kesi kama  washtakiwa 15 hawatafika siku litakaposomwa shauri hili na upande wa mashtaka mtanifanya niamini kwamba mnaitumia vibaya Mahakama," amesema Rwezile.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 23  kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 51/2018 ni Thabita Mkude, Haji Lukwambe, Emmanuel Kimoi, Mohammed Juma, Hussein Mrombo, Abdallah Hamis, Hussein Kidda, Paulo Kimoro, Brayan Morris, Hussein Nguli na Edna Kimoro.

Wengine ni  Jonathan Lema, Salha Ngondo, Ramadhan Mombo, Godwin Mwakasungura, Hassan Kibweda, Omary Hamad, Fatima Ramadhan, Ezekiel Nyenyembe, Denis Mtegwa, Dickson Kerefu, Raphael Mwaipopo, Athuman Mkawa, Mussa Kusigila,Omary Danga, Jackson Masilingi, Asha Kileta, Ally Rajabu,  Isack Ng'aga, Erick John na Aida Olomi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kuwa,  Februari 16, 2018 Kinondoni katika eneo la Mkwajuni, wilaya ya Kinondoni walifanya mkusanyiko usio wa halali na kinyume cha sheria.

Inadaiwa mkusanyiko huo ulikuwa na nia ya kufanya uvunjifu wa amani na kusababisha taharuki kwa wananchi.



Chanzo: mwananchi.co.tz