Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakala wa upinzani waapishwa Buyungu

10748 Pic+mawakala TanzaniaWeb

Wed, 8 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Mawakala wa vyama vya Chadema, ACT-Wazalendo na NRA katika jimbo la Buyungu mkoani Kigoma wamekula kiapo cha uaminifu kwa ajili ya kusimamia mwenendo wa upigaji kura, kuhesabu na kutangaza matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo hilo.

Utaratibu wa kuwaapisha unaendelea kufanyika katika makao makuu ya halmashauri ya Wilaya Kakonko ambapo vyama vilivyosimamisha wagombea vimepeleka mawakala wao watakaofanya kazi siku ya uchaguzi Jumapili.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Shaban Madede amesema tayari mawakala wa chama hicho wameapishwa na kinachosubiriwa ni kuona wakitimiza majukumu yao siku ya uchaguzi.

“Jana (juzi) tulipeleka orodha ya majina na picha za mawakala wetu kwa msimamizi wa uchaguzi lakini akayarudisha kwa makatibu wetu akidai yapelekwe kwenye kata kwa maofisa watendaji, leo (jana) wamekula kiapo wilayani,” alisema Madede.

Baada ya mawakala wake kuapishwa, chama hicho kimesema kitaendelea na mikutano yake ya kampeni kama kawaida ili kumuombea kura mgombea wao, Eliya Kanjero.

Katibu mwenezi wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Juma Ramadhan amesema mawakala wake wote wamekula kiapo japokuwa kulikuwa na changamoto.

Akizungumzia ushirikiano wa chama hicho na Chadema, alisema ni kazi ngumu kupambana na CCM bila umoja thabiti kwa vile chama hicho tawala kinatumia mabavu huku kikisaidiwa na vyombo vya dola.

Chanzo: mwananchi.co.tz