Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mavunde aahidi makubwa Dodoma

0909e7eee899aec7b09c807c50286bb3.jpeg Mavunde aahidi makubwa Dodoma

Mon, 7 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA ubunge jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amezindua kampeni na kuahidi kuharakisha maendeleo ikiwa ni pamoja na kuboresha upatikanaji huduma ya maji, kuimarisha sekta ya elimu, afya na miundombinu.

Akihutubia wananchi katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chang'ombe, Mavunde alisema akichanguliwa hatasubiri fedha za serikali kuu pekee, bali atatafuta wadau ili kusaidia kuharakisha maendeleo kwa wananchi ukiwemo upatikanaji maji katika maeneo yenye changamoto.

"Nikichanguliwa tena, nawaahidi sitasubiri fedha za serikali pekee, bali nitatafuta wadau kuharakisha maendeleo hususani katika sekta ya maji”alisema Mavunde.

Alisema mbali na ushirikiano wake na DUWASA katika kutekeleza miradi mikubwa ya kutoa maji Mzakwe na visima vya Zuzu, atahakikisha upatikanaji huduma ya maji unaimarika na kuwa mpaka kipindi cha kwanza cha ubunge, kinaisha amefanya kazi ya kuchimba visima 11.

Kuhusu elimu, Mavunde alisema kiu yake ni kuhakikisha sekta hiyo inaimarika na kuahidi kompyuta kwa shule zote za msingi na sekondari.

"Wakati namaliza ubunge wangu wa miaka mitano nimejenga shule mbili za sekondari na kujenga madarasa katika shule kadhaa za msingi na sekondari, na endapo wananchi watanipa ridhaa ya kuongoza nitaongeza kasi ya kujenga shule hususani katika maeneo ambayo wanafunzi wanalazimika kutembea muda mrefu kufuata elimu,"alisema.

Alisema pia ataboresha huduma za afya ili wananchi wa Dodoma Mjini wapate huduma bora na kuhakikisha upatikanaji wa eneo kubwa ambalo litatumika kujenga hospitali ya wilaya.

Alisema pia atendelea na mkakati wa kuwainua kiuchumi vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulamavu kwa kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya biashara na upatikanaji mikopo ili kubadilisha maisha yao.

Mavunde aliwaomba wananchi kumpa kura za ndio ili asimamie kazi ya kuhakikisha maeneo 34 ambayo hayajafikia na umeme yanafikiwa ili Dodoma iwake.

Kuhusu barabara, alisema mkakati wake ni kuhakikisha barabara zote katika kata 41 zinapitika wakati wote sambamba na kujengwaa kwa lami barabara za kuanzia Kilimani mpaka Ntyuka, na ile ya kwenda Hombolo.

Aidha, Mavunde aliwahakikishia wananchi waliopisha miradi mikubwa ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato na ujenzi wa barabaraza za mzunguko (ring road) kuwa muda si mrefu serikali itawalipa fidia baada ya kukamilika kwa ukahiki.

“Niwaombe wananchi mpigieni kura kwa Rais John Magufuli na Mbunge Mavunde na kuwapigia kura madiwani wote wa CCM ili tuweze kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi."alisema.

Mgombea ubunge Jimbo la Kibakwe, George Simbachawene aliwaomba wanaCCM na wakazi wa Dodoma kumpa kura za ndio Rais Magufuli na mgombea ubunge Mavunde kwa kuwa wamewafanyia mambo makubwa wananchi.

Alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi wa Msalato kuwa mgogoro kati ya wananchi na Magereza umeisha kwa wananchi kuhamishiwa Chihikwi.

Akizungumza kwa niaba ya watia nia 57 ndani ya CCM katika Jimbo la Dodoma Mjini, Mussa Luhambo alisema wanaungana na mgombea katika kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo kwa kufanya kazi saa 24.

Awali, aliyekuwa Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Masele alisema kutokana na utumishi mzuri wa Mavunde jimboni humo, wananchi hawana sababu ya kutompa kura zote za ndiyo.

"Mimi mwenyewe sijawahi kuwaza lakini wewe (Mavunde), umewatafutia wananchi wanyonge gari la mazishi, wewe ni kijana wa mfano na tunajivunia, Dodoma imekuwa na maendeleo makubwa sababu ya Mavunde," alisema Masele.

Chanzo: habarileo.co.tz