Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matiko akwamisha kesi ya vigogo Chadema

9770 Chadema+pic TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuwasomea maelezo ya awali viongozi wakuu wa  Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutokana na mshtakiwa wa tano, Esther Matiko kushindwa kufika mahakamani.

Akitoa udhuru ya mshtakiwa huyo leo Alhamisi Agosti 2, 2018, wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala ameieleza mahakama kuwa Matiko amepigiwa simu  ya dharura kutoka katika shule anayosoma mwanaye mjini Nairobi, Kenya na kulazimika kwenda.

Hakimu Mkazi Mkuu,  Wilbard Mashauri alimuhoji mdhamini wa mbunge huyo wa Tarime Mjini juu ya sababu za kwenda Nairobi na kujibiwa kuwa hata yeye hafahamu zaidi ya kuelezwa na Matiko kuwa  anakwenda shule anayosoma mwanaye.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi umemlaumu mdhamini  huyo kwa kutojua sababu ya kilichompeleka mbunge huyo Nairobi, kutaka akirejea awe na uthibitisho.

"Upande wa mashtaka hatuna la kufanya ila kesi itakapotajwa inabidi aieleze mahakama pamoja na udhibitisho wa nini alichoitiwa huko" amesema Nchimbi.

Nchimbi aliiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 6, 2018 huku Kibatala akiomba ipangiwe Agosti, 13, 2018 kwa kuwa Agosti 6 atakuwa na kesi Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Mashauri alikubaliana na ombi la upande wa Jamhuri na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 6.

Hakimu Mashauri pia aliwaonya wanaompigia simu, bila kuwataja majina amesema akiwa kazini anakuwa hakimu na akiwa nyumbani anakuwa Mashauri.

“Nikiwa nyumbani ni Mashauri na nikiwa kazini ni Hakimu hivyo wanaonipigia  simu nikiwa nyumbani huo sio utaratibu,” amesema hakimu Mashauri.

Mbali na Mbowe washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar); mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Musoma Vijijini, John Heche; mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Matiko.

Mbowe na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka 12 ikiwamo kuchochea ghasia, kukaidi amri ya polisi, uchochezi na uasi.

Wanadaiwa kufanya makosa hayo, Februari 16 wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana.

Katika tukio hilo, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini alipigwa risasi akiwa kwenye daladala, eneo la Kinondoni, Mkwajuni.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz