Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matawi ya CUF yavamiwa usiku, bendera zachanwa

42774 Pic+cuf Matawi ya CUF yavamiwa usiku, bendera zachanwa

Wed, 20 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unguja. Siku moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salam kufutilia mbali bodi ya wadhamini ya CUF iliyoteuliwa na Profesa Ibrahim Lipumba, watu wasiojulikana katika shehia ya Uzi mkoa wa Kusini Unguja wamevamia matawi mawili na mabaraza matatu ya wanachama wa chama hicho na kuchana bendera usiku wa kuamkia jana.

Akizungumza na Mwananchi mjini hapa jana, mkurugenzi wa siasa na habari wa chama hicho jimbo la Tunguu, Juma Ali alisema haijajulikana nani amehusika na tukio hilo kwa vile limefanyika usiku wa manane.

Alisema matawi mawili na mabaraza matatu ya wanachama wa chama hicho milingoti ya bendera zake imekatwa na na bendera kuchukuliwa na watu wasiofahamika.

“Kwa vile chama chetu kinaheshimu na kutii sheria hatutafanya lolote lile lililo kinyume cha sheria badala yake tutalifikisha suala hili sehemu husika.”

“Kwa sasa tunajikusanya kwa ajili ya kwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi Tunguu ili waweze kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria huku tukiamini kuwa waliofanya haya watadhibitiwa na kufikishwa kunakohusika,” alisema.

Baadhi ya wanachama wa CUF katika shehia hiyo walieleza kushangazwa na tukio hilo kwa vile wamekua wakifanya siasa kwa muda mrefu bila ya kugombana.

“Shehia ya Uzi ina wanachama kutoka vyama tofauti na kwa muda mrefu matukio ya kuchaniana bendera hayajatokea hivyo tunashangazwa na kitendo hiki, huenda waliofanya wamedhamiria makubwa zaidi,” alisema Ali Shaibu.

Mkurugenzi wa habari na uenezi wa chama hicho, Salim Abdallah Bimani alipoulizwa alisema amepokea taarifa hizo na kwamba anashangazwa na tukio hilo ambalo anaamini lisingeweza kutokea wakati wa sasa.

Alisema kwamba tukio hilo si la kiungwana na kuwataka wanachama wa chama hicho kutokubali kuingizwa kwenye mitego ambayo alidai kuna watu wamedhamiria kufanya uchokozi ili utokee ugomvi ambao utakuwa na madhara makubwa kwao.



Chanzo: mwananchi.co.tz