Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maspika Ndugai, Zubeir wamlilia Maalim Seif

201ea75ec9fd3041feca0d0ab5a810e9 Maspika Ndugai, Zubeir wamlilia Maalim Seif

Thu, 18 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

Spika wa Bunge, Job Ndugai ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad.

Amesema amepokea kwa masikitiko taarifa hizo na kusema taifa limepoteza kiongozi mahiri, aliyetumia muda wake mwingi kuwatumikia wananchi.

“Taifa limempoteza kiongozi mahiri ambaye alitumia muda wake mwingi kuwatumikia wananchi na kwa hakika mchango wake katika kuleta maendeleo, kudumisha amani na umoja wa kitaifa zisiwani Zanzibar utakumbukwa daima’’alisema Ndugai.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Ofisi ya Bunge jana, Spika Ndugai ametoa pole kwa familia, Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla na kumuomba Mungu awape subira na nguvu katika kipindi hiki kigumu.

Wakati huo huo, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid amesema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wamesikitishwa na taarifa za kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kilichotokea Dar es Salaam.

‘’Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa masikitiko makubwa tumepokea taarifa za kifo cha Makamo wa Kwanza wa Rais kama kilivyotangazwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na kwa mujibu wa Sheria ya Kuwaenzi Viongozi Wakuu wa Serikali, tunalazimika kuahirisha kikao cha Baraza ili kutoa nafasi ya wajumbe kushiriki katika mazishi’’alisema Zubeir.

Zubeir alisema Wajumbe wamesikitishwa na kifo cha Maalim Seif, ambaye mchango wake mkubwa katika uchumi na maendeleo, hautasahauliwa ikiwemo maridhiano ya kisiasa yaliyofungua maelewano na utulivu wa kisiasa.

‘’Kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi tunatoa mkono wa pole kwa wanachama na wafuasi wa Chama Cha ACT-Wazalendo pamoja na ndugu na familia kufuatia kifo cha Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad’’alisema.

Kikao hicho cha Baraza la Wawakilishi kimeahirishwa hadi Jumatatu wiki ijayo, ambapo Wajumbe wataendelea na mchango wa mwelekeo wa Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Wengine wamzungumzia Aliyewahi kuwa kiongozi wa juu wa Chama Cha Wananchi (CUF) kabla ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi ( CCM) na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro alisema Maalim Seif atakumbukwa kwa mambo makubwa matano.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni jabali wa siasa barani Afrika na duniani, alikuwa chuo cha siasa kinachosomwa na kujifunza wengi, alikuwa taasisi ya siasa inayojitegemea, bingwa wa maridhiano na kutaka watu wakae pamoja na alikuwa na uwezo mkubwa wa kusikiliza kuliko kuzungumza.

“Hakika tumepoteza jabali la siasa barani Afrika, hii ni pigo kwa taifa”,alisema Mtatiro ambaye aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu na Mwenyekiti wa CUF wa Mpito.

Akimzungumzia Maalim Seif, Mohamed Kikwete ambaye ni mwanachama wa CCM, alisema alimfahamu kiongozi huyo tangu mwaka 1982 hadi umauti.

Alisema taifa limempoteza kiongozi mahiri mwenye msimamo na aliyesimamia kile alichokiamini. Akizungumza na HabariLEO, Kikwete alisema Maalim Seif ni mwalimu wa wengi na amefundisha wengi.

Alisema hata yeye yapo mambo mengi amejifunza kwake, ingawa sio mfuasi wa chama, lakini vya muhimu vipo vingi kujifunza kupitia misimamo yake .

“Nimemfahamu Maalim Seif tangu mwaka 1982 tukiwa wote ndani ya CCM hadi anaondolewa chamani mwaka 1988, wakati huo yeye ni kiongozi wetu, alikuwa na msimamo na anasimamia lile analoliamini, kwa kweli tumepoteza kiongozi anayeweza kuishi na jamii ya aina yeyote vijana na wazee, ni kiongozi thabiti, hata ukifuatilia historia yake utagundua hilo”, alisema Kikwete.

Mwenyekiti wa Chama Cha ADC, Hamad Rashid Mohamed ni miongoni mwa marafiki wakubwa wa Maalim Seif wakati wakiwa CCM hadi walipoanzisha CUF miaka ya 1980.

Alisema Maalim Seif ni mwalimu wa darasani, lakini pia ni mwalimu aliyekuwa na uwezo mkubwa katika duru za kisiasa. Alisema Maalim alionesha uwezo mkubwa tangu alipokuwa CCM na kushika nafasi za juu katika Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na baadaye kufukuzwa uanachama na kwenda kuanzisha CUF mwaka 1988 na baadaye kujiunga na Chama Cha ACT-Wazalendo.

‘’Mimi nilikuwa naye katika CCM kabla ya hatujafukuzwa na kwenda kuanzisha CUF...ni mwalimu wetu katika siasa ambaye alifanikiwa kuwafundisha wanasiasa vijana katika uongozi wa vyama’’alisema Hamad Askofu wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, Dk Michael Hafidh alisema Maalim Seif alikuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla; na alikuwa na wafuasi wengi huku akiweka mbele uzalendo na mapenzi ya nchi yake.

“Ni kiongozi mwenye hekima na busara...namkumbuka siku tulipokwenda kumnasihi kumtaka asikate tamaa katika harakati za kisiasa mara baada ya kuzuiliwa kufanya kampeni kwa muda wa wiki moja... alitusikiliza na kusema yupo tayari kujenga uvumilivu wa kisiasa kwa maslahi ya taifa’’ alisema Askofu Hafidh.

Chanzo: habarileo.co.tz